Singida Big Stars yaiwashia taa Azam

25Jan 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Singida Big Stars yaiwashia taa Azam

BAADA ya ushindi wa bao 1-0 ilioupata juzi kwenye Uwanja wa Liti, Singida dhidi ya Azam FC, timu ya Singida Big Stars ni kama sasa inaitaka kwa udi na uvumba nafasi ya tatu ambayo kwa muda mrefu imekaliwa na Wanalambalamba hao.

 

Bao la Bruno Gomes, akifikisha idadi ya mabao manane kwenye orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu, liliifanya timu hiyo kufikisha pointi 43 sawa na Azam FC, ikiwa imedhidiwa mabao ya kufunga.

Azam FC iko juu kwa mabao 36 ya kufunga, huku Singida Big Stars ikiwa na mabao 24, lakini zote zikiwa zimecheza mechi 21.

Matokeo hayo hayakuwa mazuri kwa Azam FC, kwani yanaiweka kwenye hali ngumu kuipata nafasi ya tatu ambayo ni ya mwisho kwa zile zinazoipatia Tanzania mwakilishi kwenye michuano ya kimataifa.

"Nafikiri tumecheza mechi nzuri mno, na hiki ndicho ambacho makosa tunakitaka, niliwaambia wachezaji wangu kuwa tunakwenda kucheza kwa kushambulia, ingawa tumepata bao moja lakini nimefurahi," alisema Kocha Mkuu wa Singida Big Stars Hans van der Pluijm.

Nahodha wa timu hiyo Deus Kaseke alisema mechi ilikuwa na upinzani mkubwa, lakini wanashukuru kwa kupata ushindi.

"Mechi ilikuwa na upinzani mkubwa, tulitofautiana pointi tatu, tumefuata maelezo ya mwalimu tumepata matokeo," alisema.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Aggrey Morris, aliwapongeza wapinzani wao, akisema wao walifanya makosa yaliyosababisha kuadhibiwa.

"Tumefanya makosa, tunakwenda kujipanga na mechi inayokuja, timu kama haijacheza vizuri inafungwa, ila hawa ni binadamu, tunasahau tunaangalia ya mbele," alisema nahodha huyo wa zamani wa timu hiyo.

Bruce Kangwa, mchezaji wa Azam FC, alisema hayo ndiyo matokeo ya mchezaji wa mpira wa miguu, walijitahidi kila njia lakini imeshindikana, wakafungwa.

 

Habari Kubwa