Singida United: Ukata unatuyumbisha Bara

14Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Singida
Nipashe
Singida United: Ukata unatuyumbisha Bara

BAADA ya timu yake kuendelea kupoteza pointi Ligi Kuu Tanzania Bara, uongozi wa Singida United umesema tatizo kubwa linaloifanya klabu hiyo ifanye vibaya ni ukosefu wa fedha za uendeshaji.

Kauli hiyo ilitolewa juzi jioni baada ya Singida United kufungwa bao 1-0 na wenyeji Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro.

Singida United yenye pointi 33, imecheza mechi 29 na katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 20 iko kwenye nafasi ya 17 baada ya kushinda michezo nane, sare tisa na kufungwa mechi 12.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga, alisema hali hiyo inawafanya wanashindwa kuihudumia vema timu yao na kufanya maandalizi yanayostahili kabla ya kushuka uwanjani.

Sanga alisema kupungua kwa wadhamini ndiko kumechangia klabu yao "kuyumba" na kushindwa kuonyesha makali yake kama ilivyokuwa katika msimu wake wa kwanza iliposhiriki ligi hiyo wakiwa chini ya Rais wa klabu hiyo, Mwigulu Nchemba.

"Ukata unatumaliza, hali mbaya ya kiuchumi tuliyonayo inatumaliza, hatujafilisika lakini tumeyumba, kipato chetu kimepungua," alisema kiongozi huyo.

Aliongeza kuwa pamoja na changamoto hiyo, bado wataendelea kupambana kuhakikisha wanabaki kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na kurejea kwa kocha, Fred Minziro kutaongeza nguvu katika kikosi chao.

Yanga yenye pointi 67 wako kileleni katika msimamo wa ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika kila mwaka ambayo yanaandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Habari Kubwa