Singida United yajipanga kuizidi Simba kwa Kwasi

03Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Singida United yajipanga kuizidi Simba kwa Kwasi

BEKI wa kati wa Lipuli FC ya Iringa, Asante Kwasi, ameendelea kuwa lulu baada ya klabu ya Singida United nayo kuonyesha nia ya kumsajili Mghana huyo katika kikosi chake kwenye kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo, imefahamika.

Kocha wa Lipuli, Suleiman Matola.

Tayari Kwasi ambaye ameonyesha kiwango cha juu katika mechi mbalimbali alizocheza, ameshawavutia vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba na inaelezwa wameshafanya mazungumzo ya awali.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha wa Lipuli, Suleiman Matola, alisema kuwa viongozi wa Singida United,  wameshaanza mazungumzo na klabu yake kwa ajili ya kumsajili beki huyo na inavyoonekana wamejiandaa kukamilisha mchakato huo mapema baada ya Kwasi kurejea nchini.

Matola alisema kuwa licha ya kumhitaji kwenye kikosi chake, lakini anafurahi kuona wachezaji aliowafundisha kutakiwa na klabu nyingine na hiyo inaonyesha kazi yake imezaa matunda.

"Simba walikuwa wa kwanza kuja kwetu, lakini taarifa nilizopokea nyingine zinasema na Singida United pia wanamtaka Kwasi, nadhani watakaokamilisha na mchezaji atakapopendezwa atajiunga, ni fursa imetokea nasi hatuna namna," alisema Matola.

Aliongeza kuwa baada ya mapumziko mafupi aliyowapa wachezaji wake, kikosi chake kitaanza tena mazoezi kesho kwa ajili ya kuangalia wachezaji waliojitokeza kufanya majaribio na pia kujiandaa na mchezo wa mashindano ya Kombe la FA ambao utafanyika kati ya Desemba 22 na 26, mwaka huu.

Simba inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara inadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezo ya SportPesa kama ilivyo kwa Singida United ambayo yenyewe inashika nafasi ya nne.

Habari Kubwa