Singida United yawanasa Waserbia

13Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Singida United yawanasa Waserbia

KATIKA kuhakikisha inarejesha makali yake na kufanya vizuri kwenye mzunguko wa lala salama wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uongozi wa Singida United umetangaza kuwaajiri kazi makocha wawili wapya kutoka Serbia.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa timu hiyo, Frank Sanga, aliwataja makocha hao kuwa ni Popadic Dragan ambaye atakuwa Kocha Mkuu pamoja na Kocha Msaidizi, Dusan Momcilovic.

Sanga alisema kuwa wameamua kuboresha benchi lao la ufundi kwa sababu wanahitaji kuona Singida United inakuwa ni timu yenye ushindani katika kila mechi.

Alisema makocha hao wapya wataanza kazi katika mashindano ya Kombe la SportsPesa Super CUP inayotarajiwa kufanyika kuanzia Januari 22 hadi 27 mwaka huu.

Makocha wote hao wameshawahi kufanya kazi hapa nchini miaka ya nyuma na.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Singida United iko katika nafasi ya 16 ikiwa na pointi 21 baada ya kucheza mechi 19, ikishinda michezo mitano, sare sita na ikikubali kufungwa mara nane.

Habari Kubwa