Siri Taifa Stars kutoboa Afcon

11Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Siri Taifa Stars kutoboa Afcon

KUJITUMA na umakini ni moja ya vitu muhimu vinavyohitajika ili timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), iweze kufanya vema katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon)2019, zinazotarajiwa kufanyika kuanza Juni 21 hadi Julai 19, mwaka huu nchini Misri, imeelezwa.

Taifa Stars.

Akizungumza na gazeti hili jana, kiungo wa timu hiyo, Himid Mao, alisema kuwa ili waweze kupata matokeo mazuri na kusonga mbele katika fainali hizo, wanatakiwa "kujitoa kwa kiwango cha juu" na si vinginevyo.

Mao, ambaye aliungana na kikosi hicho huko huko Misri anakoitumikia Klabu ya Petrojet, alisema kuwa wachezaji wote walioko Cairo wanaendelea vema na programu ya mazoezi na wanaendelea kujifunza mbinu mbalimbali kuelekea mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

"Wachezaji wote wana ari, wana morali, tunajituma vizuri, ...tunajua hii ni michuano mikubwa, nchi yetu haijashiriki kwa muda mrefu, tunatakiwa tuhakikishe tunapigana tutoe jasho na damu ili kupata matokeo mazuri," alisema kiungo huyo wa zamani wa Azam FC.

Kikosi cha Stars kinafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Olimpiki na kabla ya kuanza kwa fainali hizo, kitacheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya Misri itakayochezwa Alhamisi mjini Alexandria na nyingine dhidi ya Zimbabwe watakayovaana Juni 16, mwaka huu.

Stars ambayo iko Kundi C itacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Segenal Juni 23, halafu itakutana na Kenya (Juni 27) na itamaliza hatua ya makundi Julai Mosi kwa kupambana na Algeria.

Habari Kubwa