Sita wawania urais wa ZFF

22May 2019
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Sita wawania urais wa ZFF

JUMLA ya wanamichezo 17 wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), utakaofanyika Juni 2, mwaka huu huku sita miongoni mwa hao wakijitosa kuwania kiti cha urais.

Kati ya waliochukua fomu hizo,  wagombea wanne wanawania nafasi ya makamu wa rais huku saba wakiwania ujumbe kutokea kila mkoa.

Katibu wa Kamati ya Uchaguzi, Omar Makungu, akizungumza na gazeti hili jana alisema mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo ulimalizika juzi Mei 20 na jana walitarajia kuanza usaili kwa upande wa wagombea wa Pemba, huku Unguja usaili ukitarajiwa kufanyika leo.

Katika nafasi za urais waliyojitokeza kuchukuwa fomu ni Khamis Abdalla Said, Suleiman Mahmoud Jabir, Ame Abdalla Dunia, Haji Ali Salum, Seif Kombo Pandu na Abrahman Mohammed Hassan.

Wanaowania umakamu wa rais,  alisema kuwa wawili wameombea Pemba ambao ni Salum Ubwa Nassor na Nassor Ali Abdallah na Unguja Ni Khamis Shaali Choum na Hussein Ahmada Vuai.

Aidha, aliwataja wagombea walioomba nafasi ya ujumbe kuwa ni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja wameomba wawili ambao ni Suleiman Haji Hassan na Faina Idarous Faina, Kaskazini Unguja kumejitokeza wagombea wawili ambao ni Seif Bausi Nassor na Rashid Tamimu Khalfan.

Mikoa iliyobakia kumejitokeza mgombea mmoja ambapo mkoa wa Kusini Unguja Ni Salum Ali Haji, Kusini Pemba ni Seif Mohammed Seif na mkoa wa Kaskazini Pemba ni Omar Ahmed Awadhi.

Habari Kubwa