Snura akiri video ya Chura 'imewavua nguo' wanawake

06May 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Snura akiri video ya Chura 'imewavua nguo' wanawake

SIKU moja baada ya Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), kupiga stop kurushwa hewani video ya wimbo wa Chura uliopigwa na msanii Snura Mushi, msanii mwenyewe ameibuka na kukiri kuwa wimbo umewadharirisha wanawake wenzake.

SNURA

Basata juzi ilitoa taarifa ya kuzuia video ya wimbo kurushwa hewani kwa madai kuwa, picha za wanawake wanaocheza wakiwa nusu uchi kwenye video hiyo ni mahitaji ya maadili.

Lakini jana, haraka haraka msanii huyo aliitisha mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam kuelezea zuio hilo la Basata.

Snura alikiri kuwa hakuwa sahihi kutengeneza video hiyo inayodhalilisha heshima na utu wa mwanamke.
Katika video hiyo, wanaonekana wanawake wakicheza kwa kukata viuno wakiwa na mavazi yaliyotoa taswira ya utupu wa mwanamke.

"Nauomba radhi umma wa Watanzania kwa jumla kwa kosa la kutengeneza, kuzindua na kuweka kwenye mtandao video ya udhalilishaji wa mwanamke, ambayo ni kinyume na maadili ya Kitanzania," alisema Snura.
Katika mkutano huo, msanii huyo aliongozana na meneja wake Hemed Kavu.

"Naviomba radhi vyombo vya serikali vinavyosimamia sanaa ya muziki kwa kosa langu la kutofuata sheria, kanuni na taratibu za sanaa ya muziki," alisema na kuongeza:

"Naahidi, mimi na meneja wangu hatutarudia tena kuandaa video kama hiyo inayolenga udhalilishaji."

Habari Kubwa