Sportpesa Cup mubashara DSTV

16Jan 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Sportpesa Cup mubashara DSTV

MICHUANO ya Sportpesa Cup inayotarajiwa kuanza Januari 22 jijini Dar es Salaam itaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Supersport ndani ya king’amuzi cha DSTV imeelezwa.

Michuano hiyo itakayofanyika kwenye uwanja wa Taifa itahusisha timu nane za Afrika Mashariki kutoka Tanzania na Kenya.

Timu hizo kwa upande wa Tanzania ni Simba, Yanga, Singida United na Mbao FC wakati kutoka Kenya ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Gor Mahia, Kariobang Shark, AFC Leopards pamoja na Bandari.

Akizungumza jana na waandishi wa habari wakati wa kutangaza rasmi ushirika huo kati ya SuperSport na SportPesa, Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania, Jacqueline Woiso, amesema kwa kuwa mshirika rasmi, SuperSport imepata idhini ya kuonyesha michuano hiyo mubashara kupitia DStv.

“Tunafurahi kuujulisha umma wa Watanzania kuwa hamu yao ya kushuhudia michuano hii mubashara kupitia DStv sasa imepatia jibu, sasa watashuhudia burudani hii ya aina yake tena kuanzia kifurushi cha chini kabisa cha Bomba” Alisema Jacqueline.

“Michezo yote itaonekana kupitia DStv SuperSport 9 ambayo inapatikana katika vifurushi vyote. Tumeamua kufanya hivyo ili kuwapa Watanzania fursa ya kushuhudia mashindano haya ambayo yanazidi kujipatia umaarufu kila uchao” aliongeza kusema Jacqueline.

Aidha kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas, amesema mashindano hayo yanazidi kukuwa na kuwa moja ya matukio makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Tangu kuanzishwa kwa michuano hii miaka mitatu iliyopita, mashindano haya yamekuwa moja ya mashindano makubwa na yanayopendwa sana kote Afrika Mashariki. Umaarufu huu unakuwa mkubwa zaidi hasa ukizingatia kuwa mshindi anapata fursa ya kucheza na timu maarufu ya Everton ya Uingereza. Kwa msingi huo, tumeamua kushirikiana na DStv kupitia SuperSport ili kuyawezesha mashindano haya kuonekana kwa mapana na marefu kwa mashabiki walio sehemu mbalimbali,” alisema Tarimba.

Mshindi wa michuano hiyo licha ya kupata nafasi ya kucheza na klabu hiyo ya England, pia atapewa zawadi ya dola za Marekani 30,000 (zaidi ya Sh. milioni 60), mshindi wa pili dola 10,000 huku mshindi wa tatu akipewa dola 7,500.

Habari Kubwa