SportPesa yaidhamini  timu ya Bunge SC

03Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
SportPesa yaidhamini  timu ya Bunge SC

KAMPUNI ya SportPesa imeikabidhi timu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vifaa vya michezo kwa ajili ya michuano ya Mabunge ya Afrika Mashariki inayotarajiwa kuanza leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa SportPesa, Tarimba Abbas (kushoto), akimkabidhi jezi na vifaa vingine vya michezo, Meneja wa Timu ya Bunge SC, John Kadutu, jijini Dar es Salaam jana. Timu hiyo inashiriki michuano ya Mabunge ya Afrika Mashariki inayoanza leo jijini Dar es Salaam. PICHA: SPORTPESA

SportPesa ambao ni wadhamini wa timu za Simba, Yanga na Singida United, walikabidhi vifaa hivyo jana kwa

Meneja wa timu ya Bunge, John Kadutu kwenye ofisi za Kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kadutu alisema SportPesa wamekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza michezo nchini na wanapaswa kupongezwa kwa hilo.

"Tunaamini kwa msaada huu wa vifaa utatuwezesha si tu kupendeza, lakini pia kufanya vizuri kwenye michuano hii inayoanza kesho," alisema Kadutu.

Aidha, kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Uwendeshaji wa Kampuni hiyo, Tarimba Abass, alisema kuwa Kampuni yake inaona fahari kuisaidia timu hiyo ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba anaamini timu hiyo itafanya vizuri katika mashindano hayo yanayofanyika nchini.

Vifaa vilivyokabidhiwa kwa timu hiyo ni pamoja na jezi, mipira, 'tracksuit' na vifaa vingine vya michezo kwa timu za mpira wa miguu, netiboli, riadha na mpira wa wavu.

Michuano hiyo inayoanza leo, inafanyika katika viwanja vya Uhuru, Uwanja wa Taifa, pamoja na Uwanja wa JK Park, huku ikitarajiwa kumalizika Desemba 11, mwaka huu.

Katika hatua nyingine kampuni hiyo leo inatarajiwa kuukabidhi Uwanja wa Taifa kwa Serikali baada ya kukamilika ukarabati wake.

Habari Kubwa