SportPesa yaidhamini tena Namungo kwa mil. 120/-

20Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
SportPesa yaidhamini tena Namungo kwa mil. 120/-

MAFANIKIO ya Klabu ya Namungo kwenye soka la Tanzania na sasa Kombe la Shirikisho Afrika, yameivutia Kampuni ya Michezo na Burudani ya SportPesa, hivyo kuamua kuongeza mkataba wa mwaka mmoja wa kuidhamini klabu hiyo kutoka Ruangwa mkoani Lindi, imeelezwa.

Namungo ambayo msimu uliomalizika ilicheza fainali ya Kombe la FA dhidi ya Simba iliyolitwaa taji hilo, imetinga hatua ya mchujo kuwania kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ambapo itacheza mechi mbili dhidi ya CD de Agosto ya Angola hapa nchini kuwania nafasi hiyo.

Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti SportPesa, Tarimba Abbas, akizungumza wakati wa kusaini mkataba wa udhamini na klabu hiyo jijini Dar es Salaam juzi, alianza kwa kuipongeza Namungo kwa kujiendesha vizuri na kuhakikisha timu inafanya vizuri barani Afrika na kuipa sifa nzuri si Tanzania pekee bali pia hata SportPesa.

“Hii ndio sababu iliyotufanya kuendelea kuwadhamini Namungo, ukiiangalia vizuri klabu ya Namungo tangu ianze mpaka sasa unaweza kuona ni jinsi gani ilivyo na moyo wa kujituma na kuhakikisha inafika mbali.

“Tunawatakia kila la kheri katika mechi zinazoendelea, kumbuka kuwa kwenye mkataba huu kuna zawadi ambazo tutawapa endapo timu itafanya vizuri katika hatua za roba fainali, nusu fainali na ubingwa," Tarimba alisema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Klabu ya Namungo, Hassan Zidadu, alisema: “Kwanza kabisa ningependa kuwashukuru sana SportPesa kwa kutupokea kwa mikono miwili na kuendeleza mkataba wetu kwa mwaka mwingine tena. Hii ni ishara ya kutukubali sisi kama klabu na kujiunga katika maendeleo yetu ili kuboresha uendeshaji wa klabu hii.

“Kama klabu tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu kwa kufanya vizuri maana nyinyi ni kama wawekezaji mkiwa na nia kubwa ya kuhakikisha klabu inajiendesha na kufikia malengo yake.

“Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika  timu imeingia kwenye hatua ya timu 32 bora barani. Mafanikio kama haya ndio yanayotufanya tuendelee kufanya vizuri na nathubutu kusema bila SportPesa tusingefika hapa. Tunajivunia sana kwa kweli.”

Huu utakuwa ni mjumuisho wa miaka miwili tangu kumalizika kwa mkataba wa kwanza kati ya SportPesa na Namungo.

SportPesa pia ni wadhamini wakuu wa Klabu za Yanga na Simba na kwa sasa wameongeza mkataba wa mwaka mmoja kwa klabu ya Namungo ambayo nayo inashirika katika Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa katika nafasi ya 13 na pointi 21 zilizotokana na mechi 16, kabla ya matokeo ya mechi za jana ambapo timu zingine zilikuwa zinacheza mechi ya 20.

Habari Kubwa