Stars kukiwasha kwa Angola leo

27Jun 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es salaam
Nipashe
Stars kukiwasha kwa Angola leo

BAADA ya juzi kuanza vizuri michuano ya Shirikisho la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa), inayoendelea nchini Afrika Kusini, kikosi cha timu ya soka ya Taifa 'Taifa Stars' leo kinatupa karata yake ya pili kucheza na Angola ukiwa ni mchezo wake wa pili katika michuano hiyo.

Stars.

Taifa Stars inayoshiriki michuano hiyo kama mgeni mwalikwa, juzi ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Malawi kwenye mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg.

Katika mchezo huo mabao ya Stars yote yalifungwa na winga Shiza Kichuya kipindi cha kwanza.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, kikosi cha Stars kinachonolewa na Salum Mayanga, kipo katika morali ya juu.

"Leo (jana) timu imefanya mazoezi mepesi tayari kuwakabili Angola na kwa mujibu wa kocha Mayanga (Salum), wachezaji wote wapo katika morali ya juu wakitaka kuhakikisha wanapata ushindi wa pili mfululizo kwenye michuano hii," alisema Lucas.

Stars inaitumia michuano hiyo ya Cosafa kuandaa timu kwa ajili ya mechi za kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).

Stars itaanza kampeni hizo kwa kucheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Rwanda Julai 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Habari Kubwa