Stars kurejea kesho, kuivaa Sudan CHAN

03Jul 2019
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Stars kurejea kesho, kuivaa Sudan CHAN

BAADA ya kupoteza michezo yake yote mitatu kwenye michuano ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, inayoendelea nchini Misri, timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars)-

Taifa Stars

- inatarajia kuwasili kesho ikitokea nchini humo tayari kuanza maandalizi ya kuwania kufuzu mashindano ya wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani barani Afrika (CHAN) dhidi ya Sudan.

Taifa Stars imepoteza mechi zote tatu za Kundi C, kufuatia kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Senegal na kisha kuchapwa 3-2 dhidi ya Kenya (Harambee Stars) kabla ya kuhitimisha kwa kulala 3-0 dhidi ya Algeria.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Cliford Ndimbo, timu hiyo itaondoka nchini Misri leo usiku moja kwa moja kabla ya kuwasili nchini kesho.

“Tunasikitika timu yetu ya taifa imepoteza tena mchezo wake wa jana, watawasili hapa nchini keshokutwa (kesho) mchana, tunaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kuipokea timu yetu ambayo ilikuwa inaitangaza nchi yetu Misri,” alisema Ndimbo.

Aliongeza kuwa wachezaji ambao walitumika katika michuano ya Afcon kuna uwezekano mkubwa wakatumika kwenye michuano ya CHAN isipokuwa wale wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi na kuwataka Watanzania wazidi kumpa kocha, Emmanuel Amunike ushirikiano.

“Nafikiri wale wachezaji ambao walitumika kwenye mashindano ya Afcon mwalimu anaweza kuwapendekeza  wakacheza katika mashindano ya CHAN ispokuwa kwa wale wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi,” alisema msemaji huyo.

Aidha, aliwataka Watanzania kuwa na subira licha ya timu yao kupata matokeo hayo na badala yake wasubiri mwalimu atakaporudi atatoa tathmini nzima ya mashindano ilivyokuwa katika michezo yote aliyocheza ikiwa ni pamoja na kuzungumzia mapungufu ya kila mchezaji.

Katika mechi ya kuwania tiketi ya kushiriki michuano ya CHAN inayotarajiwa kufanyika Januari mwakani nchini Cameroon, Taifa Stars inatarajiwa kuanzia nyumbani dhidi ya Sudan Julai 26, mwaka huu.

Cameroon imepewa nafasi ya kuandaa michuano hiyo baada ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kuinyang'anya Ethiopia wenyeji huo Aprili mwaka huu.