Stars, Tanzanite dimbani

09Dec 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Stars, Tanzanite dimbani

TIMU ya Soka ya Taifa (Taifa Stars) na ile ya wanawake ya umri chini ya miaka 20 maarufu Tanzanite Queens zinatarajia kucheza mechi za kirafiki za kimataifa dhidi ya wenzao kutoka Uganda zitakazofanyika leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mechi hizo ni maalumu katika kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema maandalizi ya mechi hizo yamekamilika ambapo mechi ya Tanzanite dhidi ya wenzao Waganda itachezwa kuanzia saa 10:30 jioni huku ile ya Stars dhidi ya Cranes ikifanyika kuanzia saa 1:30 usiku.

“Hii ni mechi za kirafiki kwa Taifa Stars na Tanzanite ambayo pia itawasaidia katika maandalizi yetu ya kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Burundi katika kusaka tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia za U-20,” alisema Ndimbo.

Alisema wageni wameshawasili na kila upande uko tayari kwa mechi hizo ambazo zitasaidia kuwaimarisha nyota wake kwa ajili ya mashindano mbalimbali watakayoshiriki.

"Kwa Tanzanite itakuwa ni sehemu muhimu kwa Kocha, Bakari Shime, kuendelea kufanyia kazi mapungufu ya kikosi chake kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Burundi utakaopigwa, Desemba 18, mwaka huu, jijini Bujumbura, ni mechi muhimu pia kwa Uganda ambao wao wanajiandaa dhidi ya Afrika Kusini," Ndimbo alisema.

Aliongeza baada ya mechi hizo za kirafiki, wachezaji watarejea kwenye klabu zao kwa ajili ya kujiandaa na mechi za raundi ya tatu ya mashindano ya Kombe la FA ambazo zitafanyika kuanzia Desemba 12 hadi 17, mwaka huu.

Habari Kubwa