Stars uwanjani tena Novemba

03Sep 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Stars uwanjani tena Novemba

KATIKA kuendelea kukijenga kikosi chake, Kocha Mkuu wa timu soka ya Taifa (Taifa Stars), Salum Mayanga, amesema watashuka tena uwanjani Novemba mwaka huu kucheza mechi mbili za kirafiki.

Salum Mayanga.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mayanga, alisema mechi hizo zitaendelea kuwajenga wachezaji wake ambao baadhi ni wapya na wanaohitaji michezo zaidi ya kirafiki ili kuwa tayari kupambana kwenye michuano mbalimbali watakayoshiriki.

Mayanga alisema kwa sasa anafurahishwa zaidi na safu ya ulinzi na nguvu amezielekeza kuimarisha eneo la ushambuliaji ili waweze kutumia vizuri nafasi wanazotengeneza katika kila mechi.

"Kwa muda mfupi wameshacheza mechi 11, ni idadi nzuri, lakini wanahitaji kupata mechi zaidi ili waweze kufikia kiwango cha juu cha kukabiliana na ushindani kutoka kwa timu yoyote tutakayokutana nayo kwenye mchezo wa mashindano," alisema Mayanga.

Kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons, aliongeza kuwa anafurahishwa na nidhamu inayoonyeshwa na wachezaji wake na kuwataka wengine ambao hajawaiwa waige mfano kwa sababu anaamini mchezaji mzuri ni yule anayetambua majukumu yake ndani na nje ya uwanja.

"Bado tuna changamoto mbalimbali kwa wachezaji wetu, lakini nawakumbusha wathamini kazi hii wanayofanya ambayo inaweza kuwaweka kwenye daraja la juu kama walivyo wanasoka wenzao wanaotamba Ulaya na hapa barani Afrika," aliongeza.

Mayanga alikabidhiwa mikoba ya kuiongoza Stars baada ya Mzalendo Boniface Mkwasa kuamua kujiuzulu huku akidai malimbikizo ya mshahara yanayofikia zaidi ya Sh.milioni 200.

Habari Kubwa