Stars yajiweka pabaya CHAN

16Jul 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
Stars yajiweka pabaya CHAN

HATIMAYE timu ya Taifa (Taifa Stars), imejiweka katika mazingira magumu ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Soka la Ndani (CHAN),-

baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Rwanda (Amavubi) katika mechi ya kwanza ya kusaka tiketi ya kucheza fainali michuano hiyo iliyopigwa jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Dominique Nshuti aliipatia Rwanda bao la kwanza baada ya kuunganisha krosi iliyopigwa na beki wa timu hiyo, Emmanuel Imanishimwe, ambaye alipiga shuti la upande wa kulia lililomshinda kipa wa Stars Aishi Manula kudaka katika dakika ya 18.

Nahodha wa Stars, Himid Mao, aliisawazishia timu yake bao kwa njia ya penalti katika dakika ya 32 baada ya beki wa Amavubi kuunawa mpira uliopigwa na Gadiel Michael wakati akijaribu kuokoa hatari kwenye lango lao.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, mchezo huo uliochezeshwa na refa Alier Michael James kutoka Sudan Kusini matokeo yalikuwa ni bao 1-1.

Mchezo huo wa kwanza wa kusaka tiketi ya kucheza fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Kenya, ulianza kwa kasi na wageni Rwanda ndio walikuwa wa kwanza kufanya shambulizi la hatari katika dakika ya 13 kupitia kwa Nshuti, lakini Gadiel wa Stars aliruka na kuokoa hatari hiyo langoni mwake huku tena beki huyo akipangua mpira uliopigwa na Mukunzi Yannick katika dakika ya 32.

Dakika ya 42 straika wa Stars, John Bocco alichelewa kuunganisha pasi iliyopigwa na Muzamiru Yassin na kumpa nafasi kipa wa Amavubi Nyayishimiye Eric kuwahi kuudaka huku kipa huyo akipangua krosi iliyokuwa inaelekea langoni mwake iliyopigwa na Boniface Maganga aliyeingia kuchukua nafasi ya Shomary Kapombe.

Amavubi ilipoteza nafasi nzuri ya kufunga baada ya mpira wa kichwa uliopigwa na Nsabimana Aimable aliyeunganisha mpira wa kona uliopigwa na Bizimana Djihadi kutoka nje katika dakika ya 72.

Stars pia ilipoteza nafasi nyingine ya kufunga baada ya kipa Ndayishimiye kupangua shuti lililopigwa na Kichuya na kutaka kuokolewa na Rucogoza Aimambe ambaye naye alitaka kujifunga dakika saba kabla ya mchezo huo haujamalizika.

Stars na Amavubi zitarudiana Jumapili Julai 23, mwaka huu jijini Kigali na mshindi wa jumla atasonga mbele katika michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2008.

Taifa Stars; Aishi Manula, Shomary Kapombe/ Boniface Maganga (dk. 17), Gadiel Michael, Salim Mbonde, Nurdin Chonya, Himid Mao, Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin, John Bocco/ Stamil Mbonde (dk. 87), Simon Msuva na Shiza Kichuya.

Rwanda; Ndayishimiye Eric, Marcel Nzazora, Bizimana Djihad, Dominique Nshuti/ Innocent Nshuti (dk. 88), Emmanuel Imanishimwe, Iradukunda Eric, Manzi Thiery, Mico Juastine/ Kayumba Soter (dk. 81), Mukunzi Yannick, Nsabimana Aimable na Barnabe Mubumbyi/ Latif Bishira (dk. 64).

Habari Kubwa