Stars yaongezewa mbinu Afcon 2019

12Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Stars yaongezewa mbinu Afcon 2019

HATUBAKI nyuma! Katika kuhakikisha kikosi cha Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), kinakuwa imara na kamili kuwakabili wapinzani wao Misri, wachezaji wa timu hiyo jana walijifunza mbinu za ushindi kupitia njia ya video.

Misri inatarajiwa kuwakaribisha Taifa Stars katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa kesho kuanzia saa 3 : 00 kwa saa za Tanzania jijini Alexandria.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi, alisema Kocha Emmanuel Amunike aliamua kutumia njia hiyo ili kubaini idara zenye nguvu na zilizo na udhaifu katika kikosi cha Misri.

Msangi alisema mazoezi ambayo wameshafanya yamewaimarisha na kila mchezaji anaonekana yuko tayari kuanza mapambano katika mechi mbili za kirafiki watakazocheza nchini humo.

"Kesho (leo) tunasafiri kuelekea Alexandria kwa ajili ya mchezo wetu wa kwanza wa kirafiki, kiujumla kambi inaendelea vema, wachezaji wako vizuri na mwalimu anaendelea kuwapa mbinu tofauti tofauti, kama jana (juzi) alitoa mafunzo kupitia video na hii alitaka kuangalia sehemu imara na dhaifu katika kikosi cha Misri ili kusaka matokeo bora," alisema Msangi.

Meneja huyo aliongeza kuwa Stars imeweka kambi katika eneo bora na wachezaji wanapata vifaa vyote muhimu vya mazoezi vinavyotakiwa na benchi la ufundi.

"Tunaamini tutapata kile tunachotarajia, maandalizi yetu ni bora na wachezaji wanaocheza kwanza wanahitaji kuweka historia katika mashindano haya, pia hawataki kuonekana walibahatisha kufika hapa," Msangi aliongeza.

Baada ya mchezo wa kesho, Taifa Stars itashuka tena dimbani Jumapili kucheza mechi nyingine ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Zimbabwe.

Inaelezwa kuwa, baada ya mechi hiyo dhidi ya Zimbabwe, Amunike atataja wachezaji wake 23 ambao ndio watapeperusha rasmi bendera ya Tanzania katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 ambazo zitaanza Juni 21 hadi Julai 19, mwaka huu.

Habari Kubwa