Stars yasogeza mbele Chalenji ya Wanawake

09Nov 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Stars yasogeza mbele Chalenji ya Wanawake

MASHINDANO ya kuwania ubingwa wa Kombe la Chalenji yamesogezwa mbele kwa muda wa siku mbili, ili kupisha maandalizi ya mchezo wa kuwania tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2021), kati ya wenyeji Timu ya Taifa (Taifa Stars), dhidi ya Equatorila Guinea, .....

Taifa Stars inatarajia kuikaribisha Equatorial Guinea Novemba 15 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicholas Musonye, alisema kuwa michuano hiyo ambayo itashirikisha nchi 10, sasa itafanyika kuanzia Novemba 16 hadi 25 mwaka huu, kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini.

Musonye alisema wameona si busara kuanza michuano hiyo, wakati wenyeji wanahitaji kujiandaa vema dhidi ya mchezo huo wa kimataifa na wanaamini, muda ulioongezeka, utazisaidia timu kuendelea kujiimarisha zaidi.

"Sasa mashindano yataanza Novemba 16, hii ni kwa sababu ya mechi kati ya Tanzania na Equatorial Guinea, mechi zote ni muhimu katika maendeleo ya soka kwenye ukanda wetu," alisema Musonye.

Alisema kuwa mechi ya ufunguzi katika mashindano hayo itakuwa kati ya wenyeji, Timu ya Taifa ya Tanzania Bara maarufu Kilimanjaro Queens dhidi ya Sudan Kusini itakayochezwa kuanzia saa 10:30 jioni, wakati mapema mchana Burundi wataivaa Zanzibar Queens.

Alieleza kuwa timu zinazoshiriki mashindano hayo zimepangwa katika makundi mawili, Kundi A likiwa na wenyeji Kilimanjaro Queens, Zanzibar Queens, Sudan Kusini na Burundi wakati Ethiopia, Kenya, Uganda na Djibouti wako Kundi B.

Aliongeza kuwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ndiyo linasaidia gharama za kuendesha mashindano hayo ya wanawake pamoja na michuano ya vijana ya umri chini ya miaka 15 (U-15) na (U-20).

Kilimanjaro Queens inayonolewa na Bakari Shime "Mchawi Mweusi" inashikilia ubingwa wa mashindano hayo mara mbili mfululizo, baada ya kushinda taji hilo mwaka 2016 mjini Jinja, Uganda na mwaka jana yalipofanyika kwenye Uwanja wa Nyamirambo jijini Kigali, Rwanda.

Habari Kubwa