Straika aipeleka Mtibwa Sugar Ligi ya Mabingwa

20Jul 2019
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Straika aipeleka Mtibwa Sugar Ligi ya Mabingwa

WAKATI akiwa katika maandalizi ya kujiandaa na msimu mpya wa mwaka 2019/20, mshambuliaji wa Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar, Stahimili Mbonde, ametoa siri ya yeye kutofanya vizuri msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Stahimili Mbonde.

Akizungumza na Nipashe jana, Mbonde, alisema kuwa  sababu iliyomfanya asifanye vizuri ni  kutoelewana vizuri na benchi la ufundi la timu hiyo.

Mbonde alisema kuwa licha ya kujituma vema kwenye mazoezi ya timu hiyo, muda mrefu hakuwa na wakati mzuri na makocha wa timu hiyo.

"Msimu uliopita sikufanya vizuri kama ilivyo kawaida yangu, sababu kubwa iliyokuwa inanikwamisha ni kutoelewana na viongozi, kwa kifupi nilikuwa na matatizo na viongozi wangu," alisema Mbonde.

Hata hivyo beki huyo wa zamani wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), alisema tayari matatizo yaliyokuwa yanamkwamisha yamemalizika, baada ya kukaa pamoja na viongozi na kuyamaliza yale yaliyokuwa yanamkwamisha.

"Nimejiandaa kurejea nikiwa imara zaidi, msimu ujao nitaonekana uwanjani kama kawaida, tayari tumeshayamaliza, ninaomba mashabiki wangu wasiwe na wasiwasi," Mbonde alisema.

Aliongeza kuwa wachezaji wote wa Mtibwa Sugar wanajifua vema kwa ajili ya kujiandaa kukabiliana na ushindani ambao watakutana nao katika msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, pamoja na mashindano ya Kombe la FA.

"Tunataka kufanya vizuri katika msimu ujao, mimi binafsi ninaahidi kurudi nikiwa na ushindani mkubwa," aliongeza mshambuliaji huyo.

Alisema kuwa wachezaji wote wa timu hiyo wamejiandaa kupata mafanikio kwa kupambana kutwaa ubingwa wa ligi au Kombe la FA ili wapate tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani.

Habari Kubwa