Straika mpya Yanga usipime

07Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Straika mpya Yanga usipime

KATIKA kuhakikisha inarejesha ufalme wake kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mbalimbali, uongozi wa Yanga umesema kuwa bado unaendelea kusajili wachezaji wenye kiwango cha juu kwa lengo la kukiimarisha kikosi chao, imefahamika.

Kauli hiyo ya Yanga imetolewa jana baada ya kumpokea mshambuliaji mpya kutoka TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Owe Bonyanga.

Straika huyo alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Kocha wa TP Mazembe, Pamphile Mihayo, kwenye mechi za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hersi Said, alisema kuwa Bonyanga, amekuja katika mazungumzo na endapo wataafikiana, atasaidia mkataba mpya wa kuanza kuitumikia timu yao.

Said alisema kuwa lengo la Yanga ni kuimarisha kikosi chao ili waweze kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano yote watakayoshiriki mwaka huu.

Alisema nyota huyo alitarajiwa kusafiri jana jioni kuelekea Zanzibar ili kuungana na wachezaji wengine wa timu hiyo ambayo leo usiku watashuka dimbani kuikabili Chipukizi kwenye mchezo wa kwanza wa Kombe la Mapinduzi.

Habari Kubwa