Sven aondoka, Simba yagawanyika mara 2

06Aug 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Sven aondoka, Simba yagawanyika mara 2
  • ***Sababu za kumtimua zawaumiza, wachezaji wapewa wiki mojai, Bodi ya Wakurugenzi sasa kuamua...

BAADA ya kukamilisha majukumu yake kwa kuibebesha Simba mataji mawili, lile la Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, hatimaye Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mbelgiji Sven Vandenbroeck ameondoka zake na kurejea kwao Ubelgiji, huku akiacha uongozi wa timu hiyo ukiwa umegawanyika mara mbili kuhusu hatima yake.

Sven ambaye mkataba wake umemalizika mwishoni mwa msimu huu, ameondoka juzi na kurejea kwao kwa mapumziko huku akiwa hajui mustakabali wa maisha yake ya baadaye ndani ya klabu hiyo kama ataongezwa mkataba ama la.

Lakini taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana kutoka chanzo chetu ndani ya Simba, uongozi wa klabu hiyo umegawanyika mara mbili kuhusu suala la kumpa mkataba mpya, huku baadhi ya wajumbe walioketi wiki hii wakitaka aendelee kuinoa Simba na wengine wakipendekeza waachane naye.

Chanzo hicho, kilieleza hadi sasa kocha huyo amekuwa akiuumiza vichwa uongozi wa klabu hiyo na kuwafanya wagawanyike mara mbili ambapo wanaotaka aongezwe mkataba wana hoja nzito wakiegemea katika mafanikio aliyoyapata msimu huu kwa kutwaa makombe mawili, huku wanaopinga wakidai kwamba alikuwa na matatizo na baadhi ya wachezaji.

“Ni kweli Sven alikuwa na matatizo yake ambayo kila binadamu anayo, ila suala hili la kuondoka au kubaki ndilo limeleta sintofahamu, huku uongozi ukitafakari vigezo ambavyo wanaweza kumuacha ilhali ameweka rekodi nzuri katika timu yetu kwa kutwaa mataji mawili chini ya uongozi wake,” kilieleza chanzo chetu bila kupepesa macho.

Kilisema kitendo cha kufanya vizuri na kutwaa mataji mawili huku timu ikicheza vizuri, kimewaweka mtegoni viongozi hao na kuwafanya watafakari mara mbili kuhusu kumwongeza mkataba au kuachana naye na kuleta mwingine.

“Muda uliobakia ni mfupi sana ukizingatia wachezaji wamepewa mapumziko ya wiki moja, kwa hali hii mchakato wa kupata kocha mwingine na timu kuanza naye maandalizi ya msimu mpya, kwa muda huo ni mdogo sana ila bado tunasubiri maamuzi ya Bodi ya Wakurugezi,” kilifafanua.

Alipotafutwa Katibu wa timu hiyo, Arnold Kashembe, alisema masuala ya kocha na benchi la ufundi yapo chini ya Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, hivyo kwa sasa wanachokifanya ni kusajili wachezaji wachache ambao wamependekezwa katika ripoti ya benchi la ufundi.

“Tumemaliza msimu tukiwa tumebeba mataji matatu, Ligi Kuu, Kombe la FA na Ngao ya Jamii, mawili yakiwa chini ya kocha wetu Sven, suala la kurejea lipo katika bodi na sasa tutasajili wachezaji ambao watasaidia timu yetu kufanya vizuri kwa msimu unaokuja ili kutetea mataji yetu,” alisema katibu huyo huku akifafanua kuwa wiki hii watageukia usajili wa wachezaji wa kimataifa.

Tayari Simba imekamilisha usajili wa wachezaji watatu wa ndani ambao ni beki wa kulia kutoka Lipuli FC, Kameta Duchu, mshambuliaji kutoka KMC, Charles Ilanfya na beki wa kati, Ibrahim Ame kutoka Coastal Union aliyesajiliwa juzi usiku kwa mkataba wa miaka miwili.

Habari Kubwa