Sven atoa mkakati wa ubingwa Simba

17Feb 2020
Isaac Kijoti
Iringa
Nipashe
Sven atoa mkakati wa ubingwa Simba
  • *** Makali ya kikosi yampagawisha akiokota tatu ugenini, huku wakielekea kuivaa Kagera Sugar kesho asema...

BAADA ya kupata ushindi wa pili mfululizo ugenini kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu, Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck ametoa siri ya kuepuka presha ya kutwaa taji hilo.

Juzi Simba ikiwa katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wao, Lipuli FC, shukrani kwa bao la dakika ya 23 kupitia kwa nahodha John Bocco.

Ushindi huo unaifanya Simba kuendelea kung'ang'ania kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 56, na 12 zaidi ya washika nafasi ya pili, Azam FC wakati huu zote zikishuka dimbani mara 22.

Hata hivyo, watani wao wa jadi, Yanga wenye mechi mbili mkononi za viporo, wapo nafasi ya tatu wakiwa na alama 39 baada ya juzi kulazimishwa sare tasa na Tanzania Prisons katika Uwanja wa Taifa wakati Azam mapema siku hiyo ikikubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union kwenye dimba la Uhuru.

Kesho Simba ikitarajia kushuka katika Uwanja wa Taifa majira ya saa moja usiku kuikaribisha Kagera Sugar, Sven ametoa siri ya kutwaa ubingwa huo bila presha.

Sven mbali ya kuwasifu wachezaji wake kwa ari waliyoonyesha dhidi ya Mtibwa Sugar wakiichapa 3-0 kabla ya juzi kuibanjua Lipuli FC 1-0, alisema wanachokitazama kwa sasa ni alama tatu tu.

Alisema wakati huu wapinzani wao wakiendelea kupoteza pointi tatu huku wengine wakiondoka na pointi moja, wao wanatazama mbele kwa kujizatiti kileleni.

Alisema ushindani ni mkubwa katika ligi hiyo, hivyo kuvuna alama tatu kutawasaidia pindi wapinzani wao watakaposhtuka watawakuta wamewaacha kwa pengo kubwa.

"Natarajia ari hii itaendelea pia katika mechi ijayo, tunataka kuendelea kuvuna pointi tatu ili kujizatiti kileleni.

"Nimefurahishwa na morali wa kikosi changu, tumepata alama tatu, sasa tunatazama mechi ijayo," alisema.

Baada ya mechi hiyo ya juzi, Simba iliondoka Iringa usiku na kulala mjini Morogoro na jana ilitarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam tayari kwa maandalizi ya kuivaa Kagera Sugar kesho kwenye mwendelezo wa ligi hiyo.

Habari Kubwa