Sven awaonya Simba wakiivaa Plateau CAF

23Nov 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Sven awaonya Simba wakiivaa Plateau CAF
  • ***Ni wakati Wanaigeria hao wakizuga kuwa hawajawa tayari, watanguliza mashushu huku akiwataka....

LICHA ya ushindi wa mabao 7-0, walioupata dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha juzi, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amewaonya wachezaji wake kutobweteka na matokeo hayo kuelekea mchezo wa mtoano wa Ligi ya....

Mabingwa Afrika dhidi ya Plateau United ya Nigeria.

Simba ambayo katika mechi hiyo ya juzi haikuwatumia baadhi ya mastaa wake akiwamo, Luis Miquisson, Chris Mugalu, Meddie Kagere, Jonas Mkude na Rally Bwalya, inatarajiwa kuifuata Plateau United Jumatano tayari kwa kushuka dimbani nchini humo Ijumaa wiki hii kabla ya timu hizo kurudiana Desemba 4, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Tayari Sven alishaeleza malengo yake kuwa ni kupata matokeo katika mechi zote mbili ya ugenini na nyumbani dhidi ya wapinzani wao hao ambao ndiyo kwanza wapo kwenye maandalizi ya msimu mpya kutokana na ligi nchini mwao kuchelewa kuanza kwa sababu ya mlipuko wa virusi vya corona.

Lakini kutokana na matokeo ya juzi, shukrani zikiwaendea mshambuliaji na nahodha wa timu hiyo, John Bocco aliyepiga hat-trick, kiungo Clatous Chama aliyetupia mawili, Hassan Dilunga 'HD' na Bernard Morrison kila mmoja akicheka na nyavu mara moja, Sven alisema juhudi na akili zao sasa wanapaswa kuzielekeza dhidi ya Plateau na kutobweteka na ushindi huo.

Sven alisema, mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa ni tofauti kabisa na huo wa Ligi Kuu na kila mchezaji anapaswa kujituma vilivyo ili waweze kutimiza malengo yao ya kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF.

"Malengo yetu ni kushinda, lakini hautakuwa mchezo mwepesi na wachezaji wanapaswa kutobeba matokeo haya," alisema Sven.

Kwa upande wa nahodha wa Simba, Bocco alisema sasa wanageukia mechi hiyo dhidi ya Plateau na wanafahamu utakuwa mchezo mgumu tofauti na mechi za Ligi Kuu, lakini wao kama wachezaji watapambana kuhakikisha wanapata matokeo.

"Kwanza niishukuru kwa kumaliza mechi hii salama na kushinda, kuhusu mechi ya Ligi ya Mabingwa natambua haitakuwa rahisi, lakini tunakwenda kupambana," alisema Bocco.

Katika hatua nyingine, taarifa zilizolifikia Nipashe jana kutoka chanzo chetu ndani ya Simba, zilieleza kuwa tayari klabu hiyo imetuma mashushu wake kwenda kuweka mambo sawa Nigeria kabla ya timu kuwasili nchini humo.

"Unajua Simba si klabu ngeni katika mashindano haya, hivyo haiwezi kwenda kichwa kichwa, tayari Abasi [Ally], ametangulia kuweka mambo sawa," Nipashe lilipenyezewa.

Hata hivyo, si Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba (CEO), Barbara Gonzalez wala Msemaji wao, Haji Manara aliyekuwa tayari kupokea simu Nipashe lilipowatafuta jana ili kuthibitisha taarifa hiyo na kuzungumzia safari ya timu hiyo kwa ujumla.

Kwa upande wa wapinzani wao, ambao wamekuwa wagumu kuzungumzia mchezo huo mara kwa mara kupitia vyombo vya habari, Ijumaa iliyopita, Kocha Mkuu wa Plateau United, Abdu Maikaba, alisema kikosi chake kitakuwa tayari kwa muda muafaka kuelekea mechi hiyo ya CAF dhidi ya Simba.

Makaiba ambaye kwa sasa na kikosi chake cha Plateau wamejichimbia mjini Aba, Kusini Mashariki mwa Nigeria, kwa ajili ya michuano midogo ya maandalizi ya msimu mpya, aliiambia Brila.net kuwa ingawa timu yake haijawa kamili vyakutosha kuelekea mechi hiyo ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa, wanapaswa kujiandaa kwa wakati kuwa fiti kwa mchezo huo.

“Hatujajiandaa vyakutosha kwa ajili ya mechi hii ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ninaamini kwa siku 10 zijazo (kuanzia Ijumaa iliyopita), tutakuwa kamili maeneo yote kwa mbinu za kutekeleza katika mechi hiyo.

“Nimewaambia vijana wangu kuwa baada ya mashindano haya (ya kujiandaa na msimu mpya), lazima tuwe tayari kwa ajili ya kuivaa Klabu ya Simba kwa sababu hatuna muda mwingi. Inaonekana kiwango chetu cha mazoezi kimwili kina alama ya maswali na natumai mchezo wa kesho (Jumamosi) utakuwa bora. "

Habari Kubwa