Sven: Mapumziko corona safi Simba

26Mar 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Sven: Mapumziko corona safi Simba

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck, amesema anajivunia mapumziko ya siku 30 kwa kudai itasaidia wachezaji wake watakaporejea kuwa fiti zaidi.

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck, picha mtandao

Akizungumza na Nipashe hivi karibuni, Sven alisema wachezaji wake walikuwa wamechoka kutokana na kucheza mechi mfululizo jambo ambalo lilikuwa likimpa wakati mgumu kwenye kupanga kikosi na kulazimika kuwapa mapumziko wachezaji wake.

Alisema watatumia muda wa mapumziko kurejea kwenye ubora kutokana na kila mmoja amempa programu ya mazoezi binafsi.

"Kwa sasa watapata muda wa kupumzika na kurejea kwenye ubora wao, Ninaamini itakuwa bora kwetu na nafuu kwani itawafanya wachezaji kuwa makini kuufukuzia ubingwa ambao tunautaka kwa sasa," alisema Sven.

Alisema alikuwa akitumia nguvu katika maandalizi yao na kuwapa mapumziko mafupi jambo ambalo lilikuwa likiwafanya wasiwe fiti kwa asilimia mia.

Simba ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 71 zilizotokana na mechi zao 28 walizocheza hadi ligi hiyo inasimama kuepuka kuenea maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19).

Habari Kubwa