Tamasha la fulldoz kufanyika leo Dar

09Sep 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Tamasha la fulldoz kufanyika leo Dar

TAMASHA kubwa la muziki lililopewa jina la 'Fulldoz' litafanyika leo kwenye Ukumbi wa Dar Live jijini Dar es Salaam huku wasanii mbalimbali wa muziki wakitarajiwa kutoa burudani ya aina yake.

Tamasha hilo linaloandaliwa na kituo cha televisheni cha ITV/ Radio One linafanyika kwa mara ya kwanza huku likishirikisha wasanii wa muziki wa aina mbalimbali.

Wasanii wanaotarajiwa kutoa burudani leo ni pamoja na msanii nguli wa muziki wa kizazi kipya, Juma Nature pamoja na Kundi la TMK Wanaume Halisi ambao wanatarajia kuwakosha mashabiki wa muziki huo wa bongofleva.

Akizungumza na gazeti hili jana, Nature, alisema kuwa wamejiandaa kufanya shoo ya aina yake kwa kuwa watakuwa kwenye maeneo yao ya nyumbani.

"Mimi nawaambia mashabiki waje wapate fulldoz katika burudani, tumejipanga kuhakikisha tunafunika na kila mtu anaondoka akiwa ameridhika na burudani yetu, sina maneno mengi ila mashabiki waje,"alisema Nature.

Msanii Q Chilla naye atatoa burudani katika tamasha hilo pamoja na bendi ya muziki wa dansi ya African Stars "Twanga Pepeta", Beka Flavour kutoka kundi la Yamoto Band pamoja na Snura.

Habari Kubwa