Tamasha la Mkeka na Mvinyo lafana Dar

18Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Tamasha la Mkeka na Mvinyo lafana Dar

HATIMAYE wakazi wa jijini Dar es Salaam wakiwa sambamba na wapendwa wao, mwishoni mwa wiki walipata fursa ya kufurahia pamoja Siku ya Wapendanao ['Valentine Day'] katika hafla maalum iliyofahamika kama ‘Mkeka na Mvinyo’ na kuvuta hisia kubwa huku waandaaji wakiahidi mambo makubwa Sikukuu ya ...

Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Uzalishaji wa Mvinyo ya Alko Vintages ya jijini Dodoma, Sweetbertha Rwabizi (kulia), akimhudumia mmoja wa wageni waliojitokeza kufurahia pamoja siku ya wapendanao yaani Valentine Day wiki iliyopita. MPIGAPICHA WETU

Pasaka, Msimu wa Sabasaba, na mwisho wa mwaka yaani 'Likizo Time'.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Hoteli ya Whitesands jijini Dar es Salaam, ilishuhudiwa wakazi hao wakijitokeza kwa wingi sambamba na wapendwa wao ili kufurahia siku hiyo maalum ambapo pamoja na vinywaji vingine waliweza kufurahia mvinyo wa aina mbalimbali unaozalishwa hapa nchini.

Mbali na burudani nzuri ya muziki laini kutoka kwa msanii Maximilian Rioba maarufu kwa jina la Milian, kivutio kingine kwenye hafla hiyo kilikuwa ni matumizi ya mikeka ambapo baadhi ya washiriki walipata fursa ya kuketi kwenye mikeka iliyoandaliwa sambamba na meza fupi wakipata vinywaji, vyakula huku wakifuatilia burudani ya muziki iliyokuwa inaendelea.

“Hii ni hafla yetu ya kwanza ya Mkeka na Mvinyo kati ya hafla nyingine nyingi za aina hii zitakazofanyika Sikukuu ya Pasaka, Msimu wa Sabasaba, na mwisho wa mwaka yaani 'Likizo Time'. Tunashukuru kuona hafla hii imepokelewa vizuri na wadau na tunawaahidi mambo mazuri zaidi yanakuja kupitia Mkeka na Mvinyo waendelee kutuunga mkono,’’ alisema Caroline Kirwanda, mratibu wa hafla hiyo kutoka Kampuni ya Real PR Solutions (RPR).

Aliwashukuru baadhi ya wadau muhimu katika kufanikisha hafla hiyo kuwa ni pamoja na kampuni ya uzalishaji wa mvinyo ya Alko Vintages ya jijini Dodoma, Hoteli ya Whitesands, Bodi ya Utalii Tanzania, (TTB), GS 1, pamoja na Kampuni ya TSN."

Kirwanda aliongeza kuwa hafla hiyo ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo utakaozinduliwa hivi karibuni unaolenga kutangaza utalii wa ndani pamoja kuvumbua fursa mbalimbali za kibiashara ndani ya nchini kwa lengo la kukuza uchumi unaofahamika kwa jina la ‘Domestic Tourism Promotion Initiative’ (DTPI).

“Tunahitaji kuhamasisha zaidi matumizi ya bidhaa za ndani ili kukuza uchumi wetu kama taifa,’’ aliongeza Kirwanda.

Kwa upande wake, Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Alco Vintages , Sweetbertha Rwabizi alisema ushiriki wao kama wazalishaji wa mvinyo wa ndani kwenye hafla hiyo unalenga kuhamasisha zaidi matumizi ya bidhaa hizo kwa kuwa tofauti na kuuza bidhaa zao pia walipata fursa ya kukutana moja kwa moja na watumiaji wa bidhaa hizo na hivyo kupata mrejesho kutoka kwao huku pia wakijenga uelewa zaidi kwa watumiaji kuhusu vinywaji hivyo.

“Iwapo Watanzania watabadilika na kuanza kutumia bidhaa hii ya mvinyo unaozalishwa hapa nchini, inaweza kukuza soko la wakulima kwa zaidi ya asilimia 80 kutokana na bidhaa hii kuzidi kupata watumiaji kadiri siku zinavyokwenda,’’ alisema.

Habari Kubwa