Tambo zatawala fainali mapinduzi

13Jan 2019
Isaac Kijoti
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Tambo zatawala fainali mapinduzi

BAADA ya safu yake ya ushambuliaji kuonekana kukosa makali katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Malindi, Kocha Mkuu wa Simba B, Nico Kiondo, amesema akiongezewa nguvu itapendeza, lakini anaamini watashinda fainali itakayochezwa leo dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Gombani.

Simba inayoundwa na wachezaji nane wa kikosi cha kwanza na wengine wakiwa wa U-20, juzi ilitinga fainali juzi baada ya kuitoa Malindi kwa mikwaju ya penalti 3-1 kufuatia dakika 90 kumalizika kwa sare tasa.

Katika mechi hiyo, penalti za Simba zilifungwa na Yusuph Mlipili, Mohammed Ibrahimu 'Mo' na Asante Kwasi, wakati Zana Coulibaly akikosa huku ile moja ya Malindi ikizamishwa kimiani na Abdulsamadu Kassim 'Haziguti'.

Baada ya kutinga nusu fainali, kikosi cha kwanza cha Simba mapema Jumatano kiljrejea jijini Dar es Salaam kwa maandalizi ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika waliyocheza jana dhdi ya JS Saoura ya Algeria.

Akizungumza baada ya ushindi huo katika Uwanja wa Amaan juzi usiku, Kiondo alisema anatambua mechi ya fainali itakuwa ngumu, lakini anaamini watapambana vyema kuweza kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ya 13 ya Mapinduzi.

"Wenzetu watakuwa na jukumu nzito kesho (jana kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa), hivyo sidhani kama wanaweza kuja kutuongezea nguvu Jumapili (leo).

"Najua watakuwa wamechoka, lakini hilo likiwezekana itakuwa vizuri, ingawa naamini pia naweza kufanya vizuri na kikosi hiki," alisema Kiondo.

Aidha, aliungwa mkono na msaidizi wake, Musa Hassan "Mgosi", ambaye alisema kucheza kwa hofu ni moja ya sababu ya washambuliaji wao kushindwa kuonyesha uwezo wao katika mchezo huo wa juzi.

"Ni suala tu la kuwajengea kujiamini, kwani tunaweza kupambambana na kutwaa ubingwa," alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba.

Kwa upande wa Kocha wa Azam, Hans van der Pluijm, aliliambia Nipashe kuwa wamejiandaa kukutana na timu yoyote na ana uhakika wa kuibebesha timu yake taji hilo.

"Unapofika fainali, lazima uwe tayari kupambana na yeyote hususan timu nzuri, sina hofu kwa hilo, tumejiandaa vizuri," alisema Mholanzi huyo.

Mechi hiyo ya fainali itachezwa kuanzia majira ya tisa alasiri, ambapo bingwa ataibuka na zawadi ya Sh. milioni 15 pamoja na kombe.

Habari Kubwa