Tamu, chungu siku 100 za Magufuli

12Feb 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Tamu, chungu siku 100 za Magufuli

RAIS John Magufuli leo anatimiza siku 100 tangu alipoingia Ikulu kuunda Serikali ya Awamu ya Tano.

Katika kipindi hicho, mambo kadhaa katika sekta ya michezo yameguswa kama sehemu ya mwendelezo wa Serikali ya Awamu ya Nne.

Lakini pia, Serikali ya Magufuli imeamua kuyaweka kipolo baadhi ya mambo yaliyofanywa na rais aliyemaliza muda, Jakaya Kikwete.

Baadhi ya mambo hayo ni kusitisha utaratibu wa kulipa mishahara makocha wa kigeni waliokuja nchini kufundisha michezo mbalimbali.

Serikali ya Kikwete ilikuwa inasaidia vyama vya michezo kuwalipa mishahara makocha wake wa kigeni, ikiwamo soka, ngumi, riadha na netiboli.

SOKA

Wakati akiondoka madarakani, Rais Kikwete aliagiza kocha wa sasa wa timu ya Taifa, Taifa Stars Boniface Mkwasa alipwe na Serikali kama ilivyokuwa kwa makocha wa kigeni.

Ingawa Serikali ya Magufuli bado haijaamua kufanya hivyo, lakini kuna vikao vinaendelea kati ya wizara husika na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mkwasa mwenye Leseni A inayotambuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), aliamua kuachana na ajira yake Yanga na kusaini miezi 18 kufundisha Stars.

MBWANA SAMATTA

Baada ya kufanikiwa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika, Rais Magufuli alimpa zawadi ya kiwanja mshambuliaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars) na klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Samatta.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ndiye alimkabidhi Samatta hati ya kiwanja hicho kilicho Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Mbali na kiwanja, Lukuvi alimpa na zawadi ya fedha, ambazo hazikutajwa kiasi chake.

MICHEZO MINGINE

Chini ya Serikali ya Rais Kikwete, michezo ya ngumi, riadha na judo ilipata makocha wa kigeni katika nyakati tofauti na kulipwa mishahara na Serikali.

Makocha wa michezo hiyo walikuwa wakitoka nchini Cuba na baada ya mikataba yao kumalizika walirejea kwao.
Sasa vyama hivyo vinaiomba Serikali kuwasaidia kama ilivyokuwa wakati wa serikali ya Kikwete.

Huku wakiwa hawana uhakika wa kukubaliwa maombi, wakati huohuo vyama hivyo vinawaandaa wanamichezo wake kwa ajili ya kushiriki michuano ya Olimpiki.

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limetakiwa kupeleka mapendekezo ya vyama vya michezo kuhusu makocha wanaowahitaji.

ATUMBUA MAJIBU

Kubwa lililofanywa hivi karibuni na Serikali ya Magufuli kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ni kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo na msaidizi wake, Juliana Yasoda.

Thadeo na Yasoda ni viongozi wa kwanza kusimamishwa kazi kwe kile kinachodaiwa utendaji mbovu ulioshindwa kuinua sekta ya michezo nchini.

Thadeo alityeuliwa kushika nafasi hiyo akitokea BMT alikokuwa katibu mkuu wa baraza hilo la Michezo.

Habari Kubwa