Tangulia Mapili, nyuma yako mbele yetu

27Feb 2016
Sabato Kasika
Dar
Nipashe
Tangulia Mapili, nyuma yako mbele yetu

MUZIKI wa dansi nchini umepata pigo tena baada ya juzi mkongwe wa muziki huo, Kassim Said Mapili kufariki dunia Alhamisi nyumbani kwake Tabata Matumbi jijini Dar es Salaam.

Marehemu Kassim Said Mapili anayepiga gita.

Kifo cha Mzee Mapili kimetokea ikiwa ni miezi mitatu tangu mkongwe mwingine wa muziki wa dansi, Kasongo Mpinda kufariki dunia mwanzoni mwa Desemba mwaka jana.

Mazishi ya gwiji hilo la muziki wa dansi nchini yalifanyika jana kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar.
Mwanamuziki huyo ameacha watoto watatu.

Mwaka jana Mzee Mapili alilazwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili katika kitengo cha moyo akiwa anasumbuliwa na matatizo la mapafu na moyo.

Matatizo hayo yalisababisha kuvimba kwa miguu yake, lakini baadaye afya yake iliimarika na kuruhusiwa kurudi nyumbani na akawa anaendelea na shughuli zake.

Mzee Mapili alizaliwa mwaka 1937 katika kijiji cha Lipuyu, tarafa ya Lionya wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.

Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Lionja, baadaye akahamia wilayani Lindi katika kitongoji cha Mtama. Akiwa huko. aliingia madrasa (shule iliyokuwa inafundisha lugha ya Kiarabu na mafunzo ya dini ya Kiislamu) kwa Sheikh Abduli Kahali.
Alikuwa miongoni mwa wapiga dufu (ngoma iliyoachwa wazi sehemu moja), ambayo mara nyingi hupigwa kwa viganja.

Mapili alikuwa na hamu ya kujiendeleza kimaisha ndipo akaachana na mafunzo hayo na kwenda mjini Lindi mwaka 1958 na kuanza kufanya biashara ndogondogo.

Akiwa katika biashara yake hiyo alianza kujifunza muziki na kuwa mwanamuziki chini ya uongozi wa Hamisi Seif Mayocha kwenye bendi ya White Jazz ya mjini Lindi.

Hata hivyo, hakudumu sana katika bendi hiyo, mwaka 1959 alihama na kwenda mkoani Mtwara kujiunga na bendi iliyojulikana kama Mtwara Jazz akiwa mwimbaji.

Baadaye mwaka 1962 aliihama Mtwara Jazz Band na kujiunga na Honolulu Jazz ya hapohapo Mtwara, lakini mwaka 1963 aliamua kurudi Lindi na kujiunga tena na bendi ya White Jazz.

Bendi hiyo ikabadili jina na kuitwa Tanu Youth League Band, ikiwa chini ya uongozi wake. Hata hivyo, Desemba 1964 alihamia Tunduru mkoani Ruvuma na kuanzisha bendi iliyojulikana kwa jina la TYL.

Kama kawaida yake, kwenye bendi hiyo hakutulia sana, alifuatwa na uongozi wa bendi ya Kilwa Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Hemed Kipande ambaye naye kwa sasa ni marehemu.

Miongoni mwa nyimbo alizotunga katika kipindi hicho ni 'Ewe Mola Tunakuomba Ubariki Afrika', 'Dunia Kukaa Wawili Wawili', 'Dolie Mimi Nakwambia', Sikutegemea' na 'Yatanikabili'.

Hata hivyo, Desemba 1965 alihamia Mgulani ambako alianzisha bendi ya JKT baada ya kununuliwa vyombo vipya vya muziki akiwa na baadhi ya wanamuziki wenzake wakiwqamo Athumani Omari, Msenda Saidi na Vinyama Kiss Rajabu.

Mapili aliendelea na utaratibu wake wa kuhama na safari hii akaangukia katika bendi ya polisi, ambayo alikaa muda mrefu baada ya kuajiriwa kama askari polisi na kupewa namba B 3710.

Akiwa katika bendi hiyo alishirikiana na wanamuziki wenzake ambao ni Omari Kayanda, Kassim Mponda, Manzi Matumla, Abdu Ali Mwalugembe, Plimo Gandam, Bosco Mfundiri, Juma Ubao na Kitwana Majaliwa.

Katika bendi hiyo, Mapili alikutana na mwanamuziki ambaye baadaye alikuja kuvuma na kuwa mashuhuri nchini, TX Moshi William, ambaye naye kwa sasa ni marehemu.

Katika bendi hiyo, Mapili aliteuliwa kuifundisha bendi ya kina mama wa Tanu Youth League, ambayo ilikuwa miongoni mwa bendi zilizokwenda nchini Kenya katika sikukuu za Kenyatta Day.

Afande Mapili alifanikiwa pia kupandishwa cheo na kuwa Koplo mwaka 1973 na kisha miaka miwili baadaye alikwenda Msumbiji na bendi hiyo ya polisi kwenye sherehe ya uhuru wa wa nchi hiyo.

Katika bendi hiyo, alifanikiwa kutunga nyimbo za 'Dunia ni Watu', 'Kashinagali Ugupina', 'Lijelalwa Ngwamba', 'Ashijajani Mweshimajani', 'Muwe Pamoja' na 'Nataka Uoe Mke Uwe Mume wa Nyumbani'.

Baada ya kutumikia bendi hiyo kwa muda mrefu, mwaka 1981 aliacha kazi na tangu wakati huo alianza kujiunga na kuongoza vyama mbalimbali vya muziki nchini.

Alihudhuria semina ya Baraza la Muziki Tanzania (BAMUTA) mwaka 1982 na akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa mpito wa chama kipya kilichoanzishwa, yaani Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA).

Mwaka wa 1984 Mapili akawa mwenyekiti wa kwanza wa CHAMUDATA. Moja ya kazi zilizofanywa na chama hicho ni kuwaleta pamoja wanamuziki 57 mwaka 1986, ambao walitunga nyimbo zilizokuwa na mafanikio ya kisiasa sio tu Tanzania bali Afrika kwa ujumla.

Miongoni mwa nyimbo hizo ni ule wa kutoa rambirambi kwa ajili ya kifo cha rais wa kwanza wa Msumbiji, hayati Samora Machel, wimbo wa miaka 20 ya kuzaliwa Azimio la Arusha na wimbo 'Fagio la Chuma' uliotamba Tanzania kipindi hicho.

Mapili ambaye alikuwa muimbaji, mtunzi na mpiga gita, alikuwa mcheshi na mpenda kutoa ushauri kwa wanamuziki wakiwamo wanaochipukia akiwahimiza wajifunze kupiga vyombo vya muziki badala ya kung'ang'ania kuimba tu.

Habari Kubwa