Tanzania bado yaiwaza Uganda

27Jun 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Tanzania bado yaiwaza Uganda

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema hivi karibuni litatoa tamko kuhusiana na rufaa waliyokata dhidi ya Uganda, ambao inadaiwa kutumia wachezaji wakubwa katika mashindano ya soka ya wanawake ya umri chini ya miaka 17, imeelezwa.

Katibu Mkuu TFF, Wilfred Kidao:PICHA NA MTANDAO

Katibu Mkuu TFF, Wilfred Kidao, alisema kuwa rufaa yao imefikia mahali pazuri na wanaamini ndani ya siku chache zijazo, watapokea uamuzi kutoka katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Kidao alisema mchakato huo unaendelea vizuri na wamejulishwa hatima ya rufaa hiyo itajulikana kabla ya ratiba mpya ya mashindano haijatolewa.

Alisema kwa sasa hawawezi kusema chochote kwa sababu suala hilo lipo katika vyombo vya sheria na wanahitaji kuwa na subira kusubiri uamuzi rasmi.

"Wiki ijayo nitatolea tamko suala zima la rufaa yetu hiyo, hapa kati tulishindwa kutokana na sababu ya janga la corona, pia suala hilo lipo chini ya mikono ya vyombo vya sheria, tusubiri majibu yao ili tuwaeleze Watanzania majibu yaliyofikiwa," alisema Kidao.

Aliwataka wadau wa soka la wanawake kuwa na subira juu ya hatima ya rufaa yao, na wanaamini uamuzi utafanyika kwa haki.

Tanzania ilikata rufaa dhidi ya Uganda kabla ya timu yake kuchapwa mabao 5-0 wakiwa ugenini wakati katika mchezo wa kwanza hapa nyumbani walipata ushindi wa mabao 2-1.

Habari Kubwa