TBF yafafanua sakata la Zonga

07Feb 2016
Faustine Feliciane
Nipashe Jumapili
TBF yafafanua sakata la Zonga

RAIS wa Shirikisho la Kikapu Tanzania (TBF) John Bandie amesema katibu mkuu wake, Salehe Zonga hajafukuzwa kazi ila amemsimamishwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhilifu wa fedha zaidi ya Sh. milioni 20 za shirikisho hilo.

Bandie aliliambia gazeti hili kuwa TBF ilikuwa na fedha kwenye akaunti yao kiasi cha Sh. milioni 38, lakini Kamati ya Utendaji imeshangazwa baada ya kukuta Sh. milioni 12 pekee.
"Zonga ndiye Katibu Mkuu anafahamu fedha zinavyoingia na kutoka kwa sababu ndiye anatia saini," alisema Bandie.
"Katika mazingira kama haya lazima tufanye uchunguzi kujua jinsi pesa zilivyotoka na hii inakwenda sambamba na kumsimamisha kwa muda kupisha uchunguzi."
Alisema kuwa matumizi waliyoyafanya TBF siyo zaidi ya Sh. milioni 10, hivyo walitegemea kwenye akaunti zingebaki Sh. milioni 20.
Uongozi wa sasa wa TBF uliingia madarakani Desemba mwaka 2013 wakiuondoa uongozi uliokuwa chini ya Rais Phares Magesa kwenye uchaguzi uliofanyika mkoani Dodoma ambapo mbali na Bandie na Zonga, pia Hamis Jafar alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.

Habari Kubwa