Tchetche aikamia Yanga

04Mar 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Tchetche aikamia Yanga
  • Straika huyo wa Azam FC kutoka Ivory Coast amefunga katika mechi zote mbili zilizopita walizokutana na Wanajangwani.

MSHAMBULIAJI tegemeo kwenye kikosi cha Azam, Kipre Tchetche, amesema anajipanga kuhakikisha anaitungua tena Yanga katika mechi ya kesho ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kipre Tchetche.

Straika huyo wa kimataifa kutoka Ivory Coast, ameifunga Yanga katika mechi zote mbili zilizopita ambazo zote walizotoka sare ya 1-1 Dar es Salaam na Zanzibar.

Pacha huyo wa Michael Bolou wa Azam FC pia, anaongoza chati ya wafumania nyavu wa timu yake msimu huu akifunga mabao tisa katika mechi 19 zilizopita za Ligi Kuu akifuatwa na John Bocco (8) na Shomari Kapombe (7).

Akizungumza na Nipashe kwa simu jana, Tchetche (28), alisema anatambua mechi ya kesho ni muhimu kwao kushinda ili kufufua matumaini ya kutwaa taji la pili la Tanzania Bara.

"Nimejipanga kufanya kile kilichotokea Zanzibar, ninawaza na kufikiria kufunga tu, na furaha yangu itazidi, nikiwafunga mabingwa watetezi," alisema.

Yanga itakuwa mwenyeji wa Azam FC ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kukusanya pointi 46 katika mechi 19 zilizopita sawa na Wanalambalamba, lakini timu hiyo ya Jangwani inabebwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Habari Kubwa