Tchetche majanga Azam FC

23Mar 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Tchetche majanga Azam FC
  • Straika huyo wa kimataifa kutoka Ivory Coast, atalazimika kufanyiwa vipimo baada ya kuumia kifundo cha mguu wakati wa mechi aliyopiga 'hat-trick' dhidi ya Bidvest Wits Jumapili.

MSHAMBULIAJI tegemeo kwenye kikosi cha Azam, Kipre Tchetche, amepewa maapumziko ya siku tatu na atalazimika kufanyiwa vipimo vya afya baada ya kuumia kifundo cha mguu wakati wa mechi yao ya Jumapili waliyoshinda 4-3 dhidi ya Bidvest kwenye Uwanja wa Azam, Dar es Salaam.

Kipre Tchetche.

Tchetche, kinara wa mabao wa Azam FC msimu huu, alipata majeraha hayo ya enka katika dakika ya 88 baada ya kufunga bao lililokamilisha 'hat-trick' yake na kushindwa kuendelea na mchezo huo na kuifanya timu yake kucheza pungufu kwa mchezaji mmoja.

Hata hivyo, uongozi wa Wanalambalamba ulisema jana kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha straika huyo hakupata majeraha makubwa katika mechi hiyo ya raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Daktari wa Azam FC, Juma Mwimbe, alisema pacha huyo wa kiungo Kipre Bolou wa Azam FC pia, alipata majeraha madogo ambayo huenda yasichukue muda mrefu kupona.

"Anahitaji kupumzika kwa siku tatu kuanzia jana (juzi) na baadaye ndiyo tutamfanyia vipimo ili kuona atatakiwa kupumzika kwa muda gani au atatakiwa kuendelea na programu za mazoezi za kawaida," alisema. "Lakini majeraha aliyopata ni madogo."

Kocha wa Azam FC, Stewart Hall,ametoa siku tatu za mapumziko kwa wachezaji wake (kuanzia juzi) kutokana na kusimama kwa Ligi Kuu Tanzania Bara kupisha mechi za Taifa Stars inayowania kufuzu kwa fainali zijazo za Mataifa ya Afrika.

Wachezaji tisa wa Azam wameitwa kwenye timu zao za taifa, saba wakijiunga na Taifa Stars, huku kiungo Jean Mugiraneza ‘Migi’ akijiunga na Rwanda 'Amavubi' na Didier Kavumbagu akikwea pipa kwenda Burundi kuungana na 'Intamba Murugamba'.

Nyota wa Azam waliojiunga na Stars itakayocheza dhidi ya Chad jijini D’jamena leo ni kipa Aishi Manula, mabeki David Mwantika, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, viungo Himid Mao, Farid Mussa na mshambuliaji John Bocco, ambaye ni nahodha msaidizi wa kikosi hicho.

Habari Kubwa