Tevez aanza kazi ya ukocha Argentina

23Jun 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Tevez aanza kazi ya ukocha Argentina

CARLOS Tevez amerejea katika soka kama kocha mkuu wa klabu ya Rosario Central ya nchini kwao, Argentina.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester United, Manchester City na Juventus, ambaye alianza na kumaliza maisha yake ya uchezaji akiwa na Boca Juniors, alistaafu mapema Juni.

Uteuzi wake na Rosario Central ulithibitishwa Jumanne huku Tevez mwenye umri wa miaka 38, akikabidhiwa kazi yake ya kwanza ya ukocha na klabu hiyo kubwa.

Tevez alishinda mataji 26 katika maisha yake ya soka na ni miongoni mwa wachezaji wanne pekee wa Argentina walioshinda Copa Libertadores (Ligi ya Mabingwa Amerika Kusini), na kunyanyua tuzo kubwa zaidi katika soka kwa klabu barani Ulaya wakati alipobeba Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na United mwaka 2008.

Alikuwa mchezaji muhimu wa timu ya Taifa ya Argentina kwa miaka mingi, akishirikiana na Lionel Messi, Sergio Aguero na Gonzalo Higuain, lakini akakosa kikosi cha Kombe la Dunia la 2014, ambapo timu hiyo ilimaliza kama washindi wa pili nyuma ya Ujerumani.

Mabingwa mara nne wa Argentina, Rosario Central walifichua Jumanne kwamba Tevez ametia saini mkataba wa mwaka mmoja, na kutangaza kwenye Twitter: "Apache anakuwa kocha mpya wa 'Dhahabu ya Bluu', baada ya kusaini mkataba na klabu kwa miezi 12."

Kabla ya Tevez kusaini mkataba wake, kipa Gaspar Servio aliiambia TNT Sports: "Kwangu mimi, ni kitu maalum ambacho Carlitos (Tevez) anaweza kuja hapa.”

Habari Kubwa