TFF kuwapiga faini mil.10 waliopanga matokeo FDL

18Feb 2016
Sanula Athanas
Nipashe
TFF kuwapiga faini mil.10 waliopanga matokeo FDL
  • *** Shirikisho hilo limebaini viashiria vya upangaji matokeo katika mechi za mwisho za ligi hiyo msimu huu zilizozihusisha Geita Gold na Polisi Tabora.

WAKATI timu za Geita Gold, Polisi Tabora, JKT Oljoro na JKT Kanembwa zinakabiliwa na adhabu ya faini ya zaidi ya Sh. milioni 10 kutoka TFF, klabu ya soka ya Mbao huenda ikapandishwa Ligi Kuu .

TIMU YA GEITA GOLD MINE

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na shirikisho hilo, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Ligi (Kamati ya Saa 72) iliyokutana juzi kupitia taarifa za mechi mbili za Kundi C la FDL -- JKT Kanembwa vs Geita Gold SC na Polisi Tabora vs JKT Oljoro, imebaini kuwapo kwa viashiria vya upangaji wa matokeo (match fixing).

JKT Kanembwa ilifungwa mabao 8-0 na Geita Gold kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma wakati Polisi Tabora ilishinda 7-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora. TFF lilisimamisha matokeo hayo hadi taarifa za mechi hizo zitakapopitiwa.

"Kwa vile suala hilo linahusisha masuala ya kinidhamu, na kwa kuzingatia Ibara ya 50(1) na (11) ya Katiba ya TFF na Ibara ya 69 ya Kanuni za Nidhamu za TFF, Kamati ya Saa 72 imemuelekeza Katibu Mkuu wa TFF apeleke suala kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya uchunguzi na hatimaye kufanya uamuzi," ilieleza sehemu ya taarifa ya TFF.

KANUNI ZAIBEBA MBAO FC Ibara ya 30(1) cha Kanuni za Ligi za TFF toleo la 2015 zilizopitishwa na kamati ya utendaji ya shirikisho hilo visiwani Zanzibar Juni 20 mwaka jana, inaipa nafasi Mbao FC kukwea Ligi Kuu kutoka Kundi C.

Timu hiyo ya Mwanza imemaliza nafasi ya nne Kundi C ikiwa na mtaji wa pointi 20 nyuma ya JKT Oljoro (22), Geita Gold (27) na Polisi Tabora (27). Ibara ya 30(1)(a) kinasema:

"Endapo timu zozote zitabainika kuwa zimepanga kwa namna yoyote ile matokeo ya mchezo wowote waliocheza kwa madhumuni yoyote yale, matokeo ya mchezo huo yatafutwa na kila timu itatozwa faini isiyopungua shilingi milioni kumi (Tshs 10,000,000).

" Kifungu (b) cha kanuni hiyo kinasema: "Viongozi wa timu hizo waliohusika na njama za kupanga matokeo watafungiwa maisha kujihusisha na masuala yoyote ya mpira wa miguu.

" Kifungu (c) cha kanuni hiyo kinaeleza kuwa timu husika hazitaruhusiwa kushiriki ligi na zitashushwa daraja, lakini ikiwa zitashindwa kulipa faini.