TFF, Serikali zatofautiana tiketi za elektoni

13Mar 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
TFF, Serikali zatofautiana tiketi za elektoni

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema kuwa tiketi za elekroniki zitaanza kutumika msimu ujao.

Jamal Malinzi

Kauli ya Malinzi inakingana na ile iliyotolewa na Serikali hivi karibuni kutaka mfumo huo kuanza kutumika mara moja.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa TFF, Malinzi, alisena agizo la Serikali kutaka mfumo huo kuanza kutumika mara moja ni gumu kutokana na upungufu uliopo.

Hata hivyo, wameshatafuta mkandarasi kwa ajili ya kupitia mfumo huo na baada ya kupata ufumbuzi watakutana na CRDB wenye mkataba na TFF kusimamia tiketi hizo.

“Mkandarasi atapitia changamoto zilizojitokeza wakati mfumo ulianza kutumika. Niseme wazi tu kuwa, tiketi za elekroniki zitaanza kutumika msimu ujao wa ligi unaoanza Agosti mwaka huu," Pia Malinzi alitumia fursa hiyo kuzungumzia ligi ya wanawake, ambayo amesema sasa itaanza rasmi mwaka sambamba na ligi ya vijana (U20).

Malinzi alisema pia msimu ujao mashindano ya Kombe la Shirikisho (Kombe la FA) yatashirikisha timu 90, badala ya 64 za msimu huu.

Naye Mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano huo wa mwaka TFF, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza aliwataka wajumbe kutumia busara zaidi katika kujadili hoja mbalimbali kwa kuzingatia soka ni ajira.

“Soka si mchezo tuu, soka ni uchumi na ajira pia. Nawaomba mawazo na fikra zenu mzielekee huko, taifa hili linawategemea.” alisema Mahiza ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa soka, netiboli na kocha.

Habari Kubwa