TFF: Shime ataiongoza Serengeti Boys Gabon

16Mar 2017
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
TFF: Shime ataiongoza Serengeti Boys Gabon

SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF), limesema hakuna mpango wa kumbadilisha kocha wa Serengeti Boys na kocha wa sasa, Bakari Shime ndiye atakayeiongoza timu hiyo kwenye fainali za Afrika za Vijana zitakazofanyika Gabon.

Bakari Shime.

Awali kulikuwa na tetesi za Shime, ambaye aliiongoza timu hiyo kufuzu kwa fainali hizo kuondolewa na kupewa nafasi ya kuwa msaidizi wa kocha wa timu ya Taifa ya Vijana 'Taifa Stars', Salum Mayanga.

Akizungumza na Nipashe juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Vijana ya TFF, Ayoub Nyenzi, alisema hakuna mpango huo na Shime yupo kambini na timu hiyo kwa maandalizi ya kuelekea Gabon.

"Shime ndiye kocha atakayeiongoza timu yetu Gabon, atakuwa na mshauri wake, Kim Poulsen, na tayari kocha yupo na vijana kambini kwa hiyo hizo tetesi si za kweli," alisema Nyenzi.

Aidha, alisema Poulsen (Kim) ameondoka nchini juzi kwenda Morocco kuandaa kambi ya timu hiyo ambayo itaenda kukaa kwa mwezi mmoja kabla ya kuelekea Gabon wiki ya kwanza ya Mei.

Serengeti Boys ipo kwenye mkakati mzito wa kuhakikisha inafanya vizuri katika fainali hizo inazoshiriki kwa mara ya kwanza.

Katika michuano hiyo, Serengeti Boys imepangwa Kundi B pamoja na timu za Angola, Mali na Niger.

Habari Kubwa