TFF yaamua basi kwa makocha makanjanja Ligi Kuu

16Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
TFF yaamua basi kwa makocha makanjanja Ligi Kuu

MAKOCHA wote wanaofundisha timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara watatakiwa kuwa na leseni A inayotambuliwa na Shirikisho la mchezo huo Afrika (CAF) ifikapo msimu wa mwaka 2018/ 2019 imeelezwa.

Jamal Malinzi

Akizungumza katika hotuba yake mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu, Rais wa TFF, Jamal Malinzi, alisema kuwa lengo la 'kuwabana' makocha hao ni kutaka kuona klabu za ligi kuu zinaongozwa na makocha wenye viwango vinavyotambulika kimataifa kwa faida ya timu husika.

Malinzi alisema kuwa hilo ni agizo na si ombi na TFF ilishatoa maelekezo ya kuhakikisha makocha wanajiendeleza kwa kipindi cha miaka mitatu.

"Kwa sasa tunataka makocha wawe na leseni B, wasaidizi wao leseni C, ila ikifika msimu wa 2018/ 2019 Kocha Mkuu wa timu ya Ligi Kuu anatakiwa awe na leseni A, nawahimiza msome hizi kozi zinazoendeshwa kila mara," Malinzi aliwaambia wajumbe wa mkutano mkuu uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Tanga.

Rais huyo alizitaka pia klabu za ligi kuu kuhakikisha zinakamilisha taratibu za kupatiwa leseni kwa sababu lolote linaweza kutokea pale waangalizi kutoka Caf au Fifa watakapokuja nchini na kutaka kufanya ukaguzi kwa timu yoyote watakayoiteua kwenye ziara yao.

Alisema kwamba ili klabu ipate leseni ni lazima iwe na ofisi, katibu wa kuajiriwa, kocha mwenye leseni inayotambuliwa, programu za timu za vijana, uwanja wa mazoezi, taratibu za kiusalama na mahesabu yaliyokaguliwa.

Wakati huo huo, Malinzi, aliwataka wanawake kujitokeza kushiriki katika kozi mbalimbali za utawala, urefarii na makocha kwa ajili ya kuongeza wigo wao wa kushiriki kikamilifu kwenye mchezo huo.

Habari Kubwa