TFF yaipandisha Mbao FC ligi kuu

24Apr 2016
Faustine Feliciane
Nipashe Jumapili
TFF yaipandisha Mbao FC ligi kuu

SHIRIKISHO la soka nchini (TFF) limeitangaza klabu ya Mbao FC ya jijini Mwanza kupanda Ligi Kuu ya Tanzania bara msimu ujao kutoka katika kundi C la Ligi Daraja la Kwanza chini iliyomalizika hivi karibuni.

Rais wa TFF Jamal Malinzi

Mbao FC imepandishwa ligi kuu baada ya kamati ya Nidhamu ya TFF kuzishusha daraja timu nne za kundi hilo kwa tuhuma za kupanga matokeo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF kupitia kwa Afisa Habari wake, Baraka Kiziguto, baada ya matokeo ya klabu za Geita Gold Mine, Polisi Tabora, JKT Oljoro, na JKT Kanembwe kufutwa Mbao FC imepata nafasi hiyo baada ya kuongoza kwenye kundi hilo kwa kuwa na pointi 12.

Mbao FC sasa inaungana na na timu za African Lyon ya jijini Dar es Salaam pamoja na Ruvu Shooting ya mkoa wa Pwani kucheza ligi kuu msimu ujao.

Wakati huo huo kikao cha Kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya TFF kinatarajiwa kukaa April, 30 Dar es salaam kujadili rufaa mbalimbali ambazo zimekatwa kutokana na maamuzi ya kamati ya Nidhamu ya TFF.

Kamati hiyo ya Rufaa ya Nidhamu ya TFF itasikiliza rufaa za Saleh Mang’ola,Yusuph Kitumbo,Amos Mwita,Fateh Remtullah,Timu ya JKT Oljoro pamoja na rufaa ya klabu ya Polisi Tabora iliyoshushwa daraja.

. Katika hatua nyingine Kamati ya Mashindano ya TFF limetangaza kuanza kwa ligi ndogo Mei 11, 2016 katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam itakayozishirikisha jumla ya timu nne.

Timu zilishoshika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi daraja la pili kwa kiula kundi Abajalo FC (Dar es salaam), Pamba FC (Mwanza), Mvuvumwa (Kigoma), Mighty Elephant (Songea) zitacheza ligi hiyo kusaka timu mbili zitakazoungana na timu nne za juu kupanda ligi daraja la kwanza (FDL) msimu ujao.

Klabu nne za Allicane Schools (Mwanza), Mshikamano FC (Dar es salaam), Mbeya Warriors (Mbeya) na Singida United (Singida) zilizoongoza msimamo wa makundi ya SDL zitaungana na timu mbili kupanda ligi daraja la kwanza msimu ujao.

Habari Kubwa