TFF: Yanga, Azam FC imekula kwenu

29Mar 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
TFF: Yanga, Azam FC imekula kwenu

BAADA ya klabu za Yanga na Azam FC kulalamikia ratiba mpya ya mechi za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema ratiba hiyo haitabadilishwa tena.

kocha wa yanga, hans van der pluijm.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa aliliambia gazeti hili jana kuwa ni kawaida kwa klabu kutoridhishwa na ratiba za mechi na wao hawana namna ya kupangua tena ratiba.

Mwesigwa alisema wamepokea barua kutoka klabu hizo wakitaka kubadilisha ratiba kwa vile inawabana kujiandaa na michuano ya klabu Afrika.

Yanga inashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na inatarajia kupambana na Al Ahly ya Misri, wakati Azam itacheza na Esperance ya Tunisia Kombe la Shirikisho.

"Bodi ya Ligi haitakuwa na nafasi ya kukutana na klabu hizo kama zilivyoomba kwa ajili ya kurekebisha tena," alisema.
Badala yake, katibu huyo amezitaka klabu hizo mbili kutumia wachezaji wake wa akiba na wale wa timu B kwa ajili ya mashindano yote wanayoshiriki na kuacha kutegemea nyota 11 peke yake.

“Kila timu imesajili wachezaji 30, pia wako wengine 20 wa U-20, sasa kwa nini inaangalia wachezaji wachache na wengine wanakaa benchi," alihoji Mwesigwa.

Katibu huyo aliongeza kuwa kwa maendeleo ya soka la Tanzania, timu hizo zinapaswa kutumia wachezaji iliowasajili na kuacha kuendelea kutumia wachache katika kila mashindano wanayoshiriki.

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, juzi aliliambia gazeti juzi kuwa waliomba kukutana na TFF kujadili suala la ratiba na ikibidi ilirekebishwe ili wapate muda wa kujiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Habari Kubwa