TFF yazidi kuneemeka

04Aug 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
TFF yazidi kuneemeka

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeingia mkataba wa haki ya matangazo ya urushaji wa mechi za Ligi Kuu Bara kwa upande wa redio na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), wenye thamani ya Sh. bilioni 3.5.

Rais wa TFF, Wallace Karia alisema mkataba huo utakuwa wa miaka 10 na shirika hilo litakuwa linaipatia shirikisho lake Sh. milioni 300 kwa kila mwaka, ambazo zitagawiwa sawa kwa klabu zote zitakazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Karia alisema kiasi kingine cha fedha kitapelekwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya soka nchini.

"Ninawapongeza TBC kwa kushinda tenda, ninaimani kuendesha mpira ni gharama, TFF itahakikisha klabu inapata gawio kwa ajili ya kuendesha timu zao, tunajua kuendesha mpira unahitaji fedha, viongozi wanatakiwa kuzitumia katika matumizi sahihi, kwa sasa ligi yetu iko kwenye nafasi nzuri, kwa Afrika tuko nafasi ya nane, hii ni jambo la kujivunia," alisema Karia.

Kiongozi huyo alisema katika ligi hakuna mkubwa, timu zote ziko sawa na mgao wote utakuwa sawa.

Naye Mratibu wa Miradi na Masoko wa TBC, Gabriel Nderumaki alisema wamefikia uamuzi huo, ili kuwapa nafasi ya Watanzania wengi kupata matangazo hayo ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa sababu ya mtandao mpana waliokuwa nayo ndani na nje ya nchi.