TFF yazikumbusha klabu, nyota Ligi Bara kujitambua

06Jul 2019
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
TFF yazikumbusha klabu, nyota Ligi Bara kujitambua

ILI kujiepusha na adhabu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limevitaka vilabu vyote nchini kuwa makini katika kufanya usajili wa wachezaji wao kwa lengo la kuepusha matatizo yanayojitokeza wakati dirisha la usajili huo litakapofungwa, imeelezwa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Ndimbo, alisema kuwa shirikisho hilo litasikitika kukuta kuna klabu imefanya usajili bila ya kukamilisha taratibu za mchakato huo ambao ndio hutoa taswira ya timu husika.

Ndimbo alisema kuwa TFF imetoa muda mrefu kama ambavyo nchi nyingine hufanya, kwa lengo la kutaka kila klabu ikamilishe mchakato huo kwa kuzingatia kanuni na taratibu.

“Tunasisitiza klabu zote zifuate taratibu za usajili, kwa sababu dirisha la usajili litakapofungwa, kusiwe na mapungufu ya baadhi ya usajili wa wachezaji kutokamilika, kila klabu iweke viambatanisho vyote muhimu, vinavyotakiwa kutokana na aina ya usajili wa mchezaji husika," alisema Ndimbo.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa, hali hiyo itasaidia kurahisisha mchakato huo, na kila mchezaji kupata timu ya kuitumikia na si kuona baadhi wanakosa klabu kwa makosa yanayojirudia kila msimu.

"Huu ni wakati wa klabu kuhakikisha mchezaji wanayemsajili, anakuwa na mkataba halali, ambao umetimia na umeridhiwa na pande zote mbili,”alisema Ndimbo.

Wakati huo huo, Ndimbo, aliwataka wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania ( Taifa Stars) ambao wamerejea nchini jana kutoka Misri kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika( Afcon) wasikatishwe tamaa na matokeo waliyopata na badala yake waelekeze akili zao kwenye mashindano yajayo.

“Vijana wetu wa Taifa Stars wamejitahidi kwa sababu ni miaka mingi tulikuwa hatujashiriki Afcon,naomba Watanzania wasiwalaumu wachezaji bali wamuachie hiyo kazi mwalimu ambaye ndio alikuwa na timu ,”alisema Ndimbo.

Taifa Stars ambayo inanolewa na Mnigeria Emmanuel Amunike sasa hivi itaanza kujiandaa mechi za kuwania tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), ambapo itaanza kwa kuwakaribisha Sudan ifikapo Julai 26 mwaka huu.

Habari Kubwa