Tigo kupeleka watano Afcon

17Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Tigo kupeleka watano Afcon

BAADA ya kuwezesha wateja wake watano kushuhudia mechi za ufunguzi za fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), kupitia promosheni yake inayoendelea ya SOKA LA AFRIKA, jana Tigo imetangaza washindi wengine watano watakaokwenda Misri  kushuhudia mechi ya fainali ya michuano hiyo.

Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael, aliwataja washindi hao kuwa ni pamoja na Kaunda Petro kutoka Zanzibar, Mohabe Senso (Dar es Salaam), Jafari Zitto, (Tanga), Shabani Msafiri (Dar es Salaam) na Lukundo Sikombe wa Arusha.

“Tigo,  tunayo furaha kuona promosheni  hii ya SOKA LA AFRIKA inawezesha wateja wetu wengine kujishindia safari ya kwenda kuona mechi za fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika sambamba na kuwezesha wateja kujishindia  fedha taslimu kwa siku, wiki na kwa mwezi kuanzia Sh. 100,000 hadi Sh. milioni 10. Vile vile tumefanikisha dhamira yetu ya kuwashukuru  kwa kuendelea kutuunga mkono kwa kununua bidhaa na kutumia huduma zetu,” alisema Shisael.

Kupitia promosheni hii itakayodumu kwa kipindi cha miezi mitatu washiriki wataendelea kujishindia zawadi za fedha taslimu kila siku, kwa wiki na kwa mwezi. Ili kushiriki kinachotakiwa ni kutuma neno SOKA kwenda namba 15670 au tembelea tovuti ya  www.tigosports.co.tz  na kujibu maswali kuhusiana na michuano hiyo ya Afcon itakayomalizika keshokutwa.

Mashindano ya promosheni ya SOKA LA AFRIKA ni sehemu ya jitihada za Tigo kuwashukuru wateja wake kwa kutumia bidhaa na huduma za kampuni hiyo. Pia promosheni hii ni sehemu ya ubunifu ambao umelenga kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha wateja.