Tiketi elektroniki zaleta tija Chamazi

16Mar 2017
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Tiketi elektroniki zaleta tija Chamazi

BAADA ya mfumo wa tiketi za kielektoniki kuonyesha tija kwa mara nyingine tena katika Uwanja wa Taifa wakati Simba na Yanga zikichuana Februari 25, mwaka huu, hatimaye zimeonyesha ufanisi mkubwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi.

Mfumo huo sasa umeonekana kuanza vyema kwenye Uwanja wa Azam Complex baada ya kutumika katika mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika, uliokutanisha wenyeji Azam FC dhidi ya Mbambane Swallows ya Swaziland.

Uwanja huo ambao awali ulikuwa ukiingiza mashabiki kwa kutumia tiketi za vishina, Jumapili iliyopita ulitumia tiketi za kieletroniki na mashabiki waliohudhuria uwanjani kuifurahia huduma hiyo na kuipongeza serikali kwa kuupanua mfumo huo hadi kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Meneja Miradi wa Kampuni ya Selcom, Gallus Runyeta, ambao ndiyo wanaosimamia mchakato huo, aliliambia Nipashe kuwa hapo kabla mfumo huo wa kisasa unaotumika kwenye Uwanja Taifa na wa Uhuru jijini Dar es Salaam, haukuwahi kutumika kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi tangu ulipoanzishwa, lakini ulivyotumika katika mchezo huo wa Kombe la Shirikisho, umefanya vizuri na uongozi wa timu hiyo unafikiria jinsi ya kuendelea kuutumia katika michuano yake mingine.

Aidha, Runyeta alisema kwa kiasi kikubwa mfumo umeweza tena kudhibiti mapato ambayo yamekuwa yakionekana kila tiketi inaponunuliwa kupitia kwa mawakala wa Selcom nchini kote au kwa shabiki kujinunulia tiketi kwa kupitia simu yake ya mkononi.

Na kwamba mfumo unauwezo wa kutunza kumbukumbu kwa kila mtu aliyenunua tiketi na unadhibiti watu wanaoingia uwanjani kwa zaidi ya asilimia 99.99,” amesema Runyeta katika ripoti ya mchezo wa Simba na Yanga wa mwishoni mwa Februari 2017.

Alisema kuonyesha mfumo huo unathibiti wezi, katika mechi ya hiyo jumla ya watazamaji 38,705 waliingia uwanjani kupitia majukwaa ya VIP na mengineyo na kiasi cha Sh. 324,810,000/- zilipatikana.

Naye Ofisa Habari wa timu hiyo, Japhar Iddy alisema kupitia tathimini fupi walioiona kwenye mchezo wao huo, wataenda kukutana kama uongozi na kujua ni jinsi gani ya kuweza kuutumia mfumo huo wa kisasa kabisa.

“Kama timu tumeukubali mfumo huu ambao hautubani katika masuala ya tiketi. Mara nyingi tumekuwa tukinunua tiketi kwa wauzaji na kuja kuziuza kwa mashabiki na tukitaraji kupata faida kupitia mauzo yetu kwa mashabiki, lakini wakati mwingine tunapata hasara kwa kununua tiketi nyingi na kuuza chache.

Lakini mfumo huu unalipwa vile ambavyo mashabiki wameingia uwanjani.

“Kwa sasa siwezi kukupa jibu la moja kwa moja kama tutaendelea na mfumo huu au kitu gani. Ni lazima tukutane na uongozi wa juu ambao utafanya tathimini yao juu ya mfumo huu na kujua jinsi gani ya kuendelea nao, lakini kama timu tumeukubali mfumo wenyewe,” alimaliza Iddy.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki waliohudhuria mechi hiyo walikiri mfumo huo ni mzuri na haukuwa na usumbufu wowote wa kuingia uwanjani kutokana na mashine kuwa nyingi na kupunguza msongamano wa mashabiki kwenye mageti ya kuingilia.

Nuhu Sadiki shabiki wa soka aliyeingia uwanjani kutumia mfumo huo alisema mfumo huo wa kisasa ni mzuri na wa kuungwa mkono ili timu ziweze kuendelea kimaendeleo.

“Mfumo huu hauna shida kama ukiwa na mashine nyingi kama ilivyo leo (Jumapili iliyopita). Tumeingia uwanjani katika hali nzuri na hakukuwa na msongamano milangoni na kila mtu aliingia kwa utaratibu mzuri ambao umewekwa na nashauri utaratibu huu uwekwe na Uwanja Taifa ili mashabiki wasiwe wanalalamika.

Dunia ya leo hivi ndivyo ilivyo na inahitaji mambo kama haya ili timu, taasisi zipate mafanikio. Tukisema hatuwezi, itabidi tujiulize ni lini tutaweza,” alisema Nuhu.

Habari Kubwa