Tiketi elektroniki zazua utata wa mapato

07Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Tiketi elektroniki zazua utata wa mapato

WAKATI serikali ikisisitiza matumizi ya tiketi za elektroniki kwenye Uwanja wa Taifa na Uhuru jijini Dar es Salaam, mapato kwenye viwanja hivyo yanazidi kupungua tofauti na mikoani yanakoongezeka.

Kiongozi mmoja wa juu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) aliliambia Lete Raha kuwa hali ya mapato sasa imebadilika na shirikisho hilo limekuwa likiingiza kiasi kikubwa cha fedha kwenye mechi za mikoani ambazo bado wanatumia tiketi za vishina.

"Mechi kati ya Yanga na Azam ambayo ilitarajiwa kuingiza kiasi kikubwa cha pesa badala yake kilichopatikana ilikuwa ni Sh. milioni 34 kwenye Uwanja wa Taifa wakati Mbeya City dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya zaidi ya Sh. milioni 60 zilipatikana," alisema kiongozi huyo.

Aliongeza kuwa mechi kati ya Stand United dhidi ya Simba iliyofanyika Jumatano iliyopita mkoani Shinyanga iliingiza Sh. milioni 45 kiasi ambacho ni kikubwa sana ukilinganisha na mapato ya mechi ya Yanga dhidi ya Azam.

"Watu hawapendi shida, mtu anataka aingie uwanjani bila karaha, tiketi za mashine zimeonekana zimekuja haraka, elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa wananchi," aliongeza kiongozi huyo.

Alisema mfumo huo mpya unatakiwa kurekebishwa mapema endapo serikali itatoa ruhusa na mechi ya marudiano kati ya Simba na Yanga ifanyike kwenye Uwanja wa Taifa mwakani.

Habari Kubwa