Timu ya vijana yaifunga Moro Kids 3-1 Jamhuri

10Dec 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Timu ya vijana yaifunga Moro Kids 3-1 Jamhuri

TIMU ya taifa ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 15, imemaliza ziara yake mkoani Morogoro kwa mafanikio baada ya juzi Alhamsi Desemba 8, kuifunga Moro Kids mabao 3-1 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Kwa siku ya jana Ijumaa Desemba 9, mwaka huu timu hiyo ilijifua kwa mazoezi kwa mujibu wa programu ya Kocha Oscar Mirambo baada ya Morogoro kuleta timu ya wakubwa tofauti na vijana wenye umri wa chini ya miaka 15. Hivyo, mchezo huo wa pili haukufanyika.

Mazoezi na michezo hiyo ya kirafiki ambayo mingine wataifanya Zanzibar juma lijalo, ni maandalizi ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Burundi mchezo unaotarajiwa kufanyika Desemba 18, mwaka huu kwenye Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.

Awali ilipangwa icheze na Shelisheli ambayo imetoa taarifa ya kuwa haijajiandaa.

Mara baada ya Morogoro, timu hiyo imerejea Dar es Salaam leo kujiandaa na safari ya kwenda Zanzibar Desemba 11 ambako itakuwa na michezo miwili mingine ya kirafiki.

Zanzibar itacheza na Kombaini ya timu ya Vijana wa Zanzibar Desemba 12, 2016 kabla ya kurudiana Desemba 14, mwaka huu na timu hiyo na Kombaini kabla ya kurejea Bara Desemba 15, kujiandaa na mchezo kirafiki wa kimataifa dhidi ya Shelisheli.

Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu wa timu ya vijana weeny umri wa chini ya miaka 14, Oscar Mirambo anayepata ushauri kutoka kwa Mshauri Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana, Kim Poulsen kinaundwa na makipa ni Shaban Hassan Kimwaga na Abdulatif Noor Lema.

Walinzi ni Kareem Bakari Mfaume, Asante Hamis Bwatam, Rashid Hamisi Rashid, Moris Michael Njako, Harubu Juma Tanu, Cosmas Lucas Jakomanya, Salim Abubakar Lupepo na Dastan Daniel Matheo.

Viungo ni Edson Jeremiah Mshirakandi, Jonathan Raphael Kombo, Alphonce Mabula Msanga, Erick Boniface Bunyaga, Gasper Godfrey Gombanila, Sabri Dahari Kondo na washambuliaji ni Jafari Juma Rashid, Ludaki Juma Chasambi, Steven Emmanuel Sodike, Michael Mussa Mpubusa na Edmund Geofray John.

Timu hii inaundwa na vijana ambao TFF iliwakusanya tangu 2014 na kuwaunganisha kwa pamoja katika Shule ya Msingi na Sekondari ya Kukuza Vipaji ya Alliance iliyoko Mwanza.

Mbali ya kutoa elimu ya msingi na sekondari, pia Alliance inatoa elimu ya awali kwa watoto wa kuanzia umri wa miaka miwili hadi sita.

Timu hii inaandaliwa kuja kwa muda mpya wa Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ambao watashiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana mwaka 2019 ambako Tanzania imeteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa mwenyeji.

Kambi itavunjwa Desemba 18, mwaka huu.

Habari Kubwa