Toto wamtimua mwenyekiti, kisa ni mwanachama wa Yanga

06May 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Toto wamtimua mwenyekiti, kisa ni mwanachama wa Yanga

KLABU ya Toto Africans, imemtimulia mbali Makamu mwenyekiti wake, Waziri Gao baada ya kubaini kuwa ni mwanachama halali wa klabu ya Yanga, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya katiba ya timu hiyo ya Mwanza.

TOTO

Uamuzi huo ulifikiwa na kamati ya utendaji ya timu hiyo siku chache baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu hiyo ya Mwanza katika mechi ya Ligi Kuu Bara wiki iliyopita.

Akizungumza na Nipashe jana, Gao alikiri kuwa yeye ni mwanachama halali wa Yanga kwa miaka 10 na taarifa za kutimuliwa kwake ni kweli.

"Ni kweli uamuzi nimetimuliwa kwa kusema kwangu ukweli. Mimi ni mwanachama wa Yanga kwa miaka 10," alisema Gao na kuongeza:

"Nimekuwa hapa Toto kwa miaka minne, nakiri kuondolewa lakini lengo langu halikuwa baya, nilitaka kuisaidia Toto."
Alisema kimsingi amekubalina na uamuzi wa kamati ya utendaji kwa sababu ni kinyume na katiba ya Toto.

"Nimekuwa mkweli mbele ya soka la Tanzania, nimeamua kuweka wazi uanachama wa klabu ya ya Yanga," alisema.
Alisema pamoja na kuondolewa Toto, anaamini kuna watu wengi kwenye timu hiyo wenye mapenzi na klabu kubwa za Yanga na Simba.

"Nitakuwa tayari kuisaidia Toto pale watakapoitaji msaada, nimefanya kazi kuhakikisha Toto haishuki daraja na ndio maana tulifanikiwa kupata pointi tatu kwa Simba na pointi moja kwa Azam ambazo kwa kiasi kikubwa zimetusaidia kuondoka kwenye hatari ya kushuka daraja," alisema Gao.

Habari Kubwa