Tshishimbi aiita Simba mezani

26Mar 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Tshishimbi aiita Simba mezani
  • ***GSM yajiweka kando Yanga, asema hata Azam ikifika dau anakwenda, huku....

WAKATI nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi akiwaita mezani Simba, hali ndani ya klabu hiyo imekuwa 'tete' baada ya Kampuni ya GSM kutangaza rasmi itajiweka pembeni kufanya shughuli mbalimbali za uendeshaji ambazo haziko kwenye mkataba, imefahamika.

Kiungo wa Yanga, Papy Tshishimbi, anayeelezwa kuingia katika mawindo ya watani zao, Simba. PICHA: MAKTABA

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Tshishimbi alikiri kufanya mazungumzo na Yanga na kupokea nakala ya mkataba mpya, lakini bado hajasaini kwa sababu klabu hiyo haijatimiza dau ambalo analitaka.

Tshishimbi alisema mpira ndio kazi yake na yuko tayari kujiunga na Simba, Azam au Namungo endapo watafikia dau lake analolitaka atasaini na kwenda kuitumikia.

"Mkataba wangu ulikuwa ni wa mwaka mmoja, unamalizika mwezi wa nane, nimebakiza miezi minne tu, wameshaniletea mkataba mpya, ila kuna mambo bado tunaongea, tunazungumza, wakiwa tayari tutamalizana, mimi sichagui," alisema Tshishimbi.

Aliongeza kuwa ana familia, hivyo anahitaji kusaini mkataba ambao utakuwa mnono kwake kwa sababu kila mmoja kwenye kazi yake anahitaji mafanikio.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya klabu ya Yanga zinaeleza kuwa Tshishimbi amegoma kusaini mkataba mpya baada ya kusikia mshambuliaji Bernard Morrison amepewa donge nono, lakini chanzo kikingine kilieleza kwamba tayari alishasaini mkataba wa awali wa kujiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba.

Aidha, kuhusu tamko la GSM limetolewa siku chache baada ya kampuni hiyo kukamilisha mchakato wa kumwongezea mkataba mpya wa miaka miwili Morrison, ambaye alitajwa kuwindwa na watani zao, Simba.

Kwa mujibu wa barua ya GSM iliyopatikana jijini jana kwenda kwa uongozi wa Yanga ambayo iliandikwa juzi, Machi 24, mwaka huu na kusainiwa na mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Feisal Mohammed, inasema sasa haitafanya jambo lolote ambalo lipo nje ya mkataba.

Taarifa ya kampuni hiyo ilitaja shughuli ambazo ilizifanya kwa mapenzi ya kurejesha heshima ya klabu hiyo bila ya kuwapo kwenye mkataba kuwa ni pamoja na kumrudisha kikosini beki, Lamine Moro ambaye alikuwa ameondoka baada ya kutangaza kukatiza mkataba wake, kuwasajili Morisson, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima na Adeyum Saleh kwa lengo la kukiongezea nguvu kikosi chao wakati wa dirisha dogo.

Wadhamini hao pia wameeleza kuwa walilipa gharama za kumleta Kocha Mkuu, Luc Eymael na wasaidizi wake, mishahara, usafiri wa ndani, nyumba na tiketi za kwenda na kurudi makwao za makocha hao huku pia wakilipa mishahara ya wachezaji na bonasi za ushindi katika mechi zote walizoshinda tangu Desemba mwaka jana.

Kampuni hiyo pia ilitoa ahadi ya Sh. milioni 200 endapo wataifunga Simba, ahadi ambayo imeshatekelezwa baada ya ushindi wao wa bao 1-0, wamelipia gharama za kambi, usafiri wa ndege wa timu kuelekea katika baadhi ya mechi na kugharamia uwanja wa mazoezi, ukarabati wa uwanja, ununuzi wa vifaa vya mazoezi na kulipa baadhi ya madeni ya nyuma ya usajili wa wachezaji.

"Haya yote yamefanyika kwa mapenzi mema kwa klabu yetu bila kujali gharama nyingi na kubwa tunazolipa, pia katika kuelekea mabadiliko ya kiundeshaji wa klabu, GSM ilitafuta wataalamu kuja kushauri na kusaidia mabadiliko ya kimfumo na kupata timu rafiki kubwa ya barani Ulaya (Benfica)," ilisema sehemu ya barua hiyo.

Iliongeza kuwa, wanasikitika kusikia baadhi ya viongozi wakisema kampuni hiyo inawaingilia viongozi na sasa itafanya shughuli ambazo ziko kwenye makubaliano tu.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alipoulizwa kuhusu barua hiyo ya GSM, alisema haijafika klabuni kwao na wao wanaamini wataendelea kushirikiana vema na kampuni hiyo kama ilivyokuwa awali.

Bumbuli alisema anaamini kila kitu kitakwenda vizuri na hakuna mwanachama yeyote wa klabu hiyo yuko tayari kuona mambo yanakwenda 'kombo'.

Habari Kubwa