Tshishimbi amwaga mboga rasmi Yanga

01Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Tshishimbi amwaga mboga rasmi Yanga
  • ***Ashangaa kupewa siku 14 kupitia redioni, amponda Kaimu Katibu Mkuu, asema hajaua kwao hivyo yupo tayari...

SAKATA la usajili wa Kiungo Papy Tshishimbi limezidi kuchukua sura mpya baada ya mchezaji na nahodha huyo wa Yanga kuibuka na kudai kuwa hajaua mtu kwao, hivyo kama klabu hiyo haimtaki yupo tayari kurejea nyumbani ama kutafuta timu nyingine.

Aidha, Tshishimbi ‘amemponda’ Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Wakili Patrick Simon, kwamba licha ya kuwa mwanasheria hajui mambo ya soka kutokana na kwenda kuuzungumzia mkataba wake kupitia redio moja jijini Dar es Salaam.

Awali katika sakata hilo, kiungo huyo alisema bado hajasaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo, na alipoulizwa Simon juzi, alikiri ni kweli na kwamba wamempa siku 14 Mkongomani huyo kufanya uamuzi kuhusu hatima yake ya kusaini ama la.

Simon alisema: "Alifanya mazungumzo na makubaliano yalifikiwa, bado tu kusaini mkataba mpya, baada ya mazungumzo hayo,
Hersi Said (GSM) alitueleza viongozi, lakini uongozi wa klabu nao ulitoa mapendekezo yake juu ya kiasi anachokitaka Tshishimbi na tulisema tukipunguze na tumempa siku 14 ambazo zitamalizika Jumatano wiki ijayo," alisema kiongozi huyo.

Lakini baada ya taarifa hiyo, Tshishimbi ameibuka na kumponda kiongozi huyo kwa hatua ya kuuzungumzia mkataba wake redioni huku akishangaa kuambiwa amepewa siku 14 kitu ambacho hajaelezwa.

"Hajui mambo ya mpira (Naibu Katibu Mkuu, Simon Patrick) ingawa ni mwanasheria hawezi kwenda kuzungumzia mkataba wangu redioni, hata hivyo kwetu sijaua mtu, kama hawanitaki naweza kurudi ama kutafuta timu nyingine," alisema Tshishimbi.

Alisema Yanga kama wanataka wao wachukue maana uamuzi ni wao na yeye atatafuta timu nyingine ama kuamua kurejea kwao kabisa.

Kwa mujibu wa Simon, Yanga haina muda wa kuendelea kuvutana na mchezaji mmoja na imemtaka kutoa uamuzi wa kusaini mkataba huo ama, vinginevyo ipo tayari kutazama kwingineko katika kuziba pengo hilo kwa kuwa inaamini wapo wachezaji wengi wazuri wa nafasi hiyo.

"Jukumu lipo kwake ikiwa ataridhika na mkataba tuliompa, atasaini," alisema Wakili Simon huku akieleza Yanga ni taasisi kubwa na hakuna mchezaji au kiongozi ambaye yuko juu ya klabu hiyo, hivyo kazi zote zinafanywa kwa kufuata taratibu.

Habari Kubwa