TTA kazini kusaka timu ya Taifa ya Wanaume

11Sep 2021
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
TTA kazini kusaka timu ya Taifa ya Wanaume

CHAMA cha Mchezo wa Tenisi Tanzania (TTA), kimesema kwa sasa kinaendelea na mchakato wa kusaka vipaji kwa ajili ya kuunda timu ya Taifa ya Wanaume, inayotarajiwa kushiriki mashindano ya dunia mwakani.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa TTA, Denis Makoi, alisema awali walifanikiwa kupata timu ya Taifa ya Wanawake na sasa mchakato unaofuata ni wa kusaka timu ya wanaume ambao unatarajiwa kufanyika jijini Arusha mwezi ujao.

“Kwa sasa tupo kwenye mchakato wa kutafuta timu ya Taifa ya Wanaume kwa ajili ya kujiandaa kushiriki mashindano ya dunia, zoezi hilo litafanyika mwezi ujao. Kwa upande wa timu ya Wanawake tayari tumepata kwa sasa wanaendelea kufanya mazoezi,” alisema Makoi.

Mwenyekiti huyo alisema kwa upande wa Tanzania ni mara ya kwanza kwenda kushiriki mashindano makubwa kama hayo, hivyo wanawapa mbinu wachezaji wao kwa kuangalia jinsi nchi nyingine zinavyofanya kwenye mashindano ya miaka iliyopita.