Twiga Stars kulipa kisasi kwa Zimbabwe leo?

04Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar
Nipashe
Twiga Stars kulipa kisasi kwa Zimbabwe leo?

TWIGA Stars itakuwa mwenyeji wa timu ya taifa ya wanawake wa Zimbabwe (Mighty Warriors) katika mchezo wa kwanza wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (AWC) kwenye Uwanja wa Azam, Dar es Salaam leo jioni.

Twiga Stars.

Stars itaingia uwanjani leo ikisaka kisasi cha kutolewa kwa matuta 4-2 na Wazimbabwe hao katika mashindano ya Cosafa baada ya kutoka sare katika muda wa kawaida wa dakika 90 mwaka juzi.

Kocha wa Twiga Stars, Nasra Juma, aliiambia Nipashe jana kuwa kikosi chake kimejipanga kushinda leo na kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.

"Tunawaheshimu Zimbabwe kwa sababu wana timu nzuri, ndani ya miaka minne tumeshacheza nao zaidi ya mara nne, upungufu uliyojitokeza katika michezo iliyopita tumeufanyia kazi na kesho (leo) ni nafasi yetu ya kulipa kisasi," alisema Nasra.

Kocha huyo aliyerithi mikoba ya Rogasian Kaijage, aliyejiuzulu, alisema wachezaji wake wameahidi kupambana kuwang'oa wapinzani wao.

Nahodha wa Twiga Stars, Sophia Mwasikili, alisema kila mchezaji yuko tayari kupambana na kuhakikisha wanamaliza 'uteja' dhidi ya Zimbabwe.

"Tuko vizuri, tumefanya mazoezi ya aina mbalimbali, walimu wetu walikuwa wanatukumbusha mambo muhimu ya kufanya kuelekea mchezo huu, na sisi pia tunajua nini wenzetu wanatuzidi, hatutaki kurudia makosa," alisema.

Timu hizo mbili zitarudiana baada ya wiki mbili mjini Harare na timu itakayosinga mbele itachuana na Zambia katika hatua itakayofuata.

Habari Kubwa